Kampuni mbili zatakiwa kuwalipa wakulima wa pamba Sh362 milioni

Mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu akiongea na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo. Picha na Anthony Mayunga.

Muktasari:

Kampuni mbili za pamba Wilaya ya Serengeti zinadaiwa Sh362 milioni na wakulima tangu kuanza kwa msimu mpya wa zao hilo.

Serengeti. Kampuni mbili za pamba Wilaya ya Serengeti zinadaiwa Sh362 milioni na wakulima tangu kuanza kwa msimu mpya wa zao hilo.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 23, 2019 katika mkutano wa baraza la madiwani, mkuu wa Wilaya ya Serengeti,  Nurdin Babu amesema kampuni ya CS and C inadaiwa Sh300 milioni wakati ile ya Oram ikidaiwa Sh62 milioni.

Amesema kampuni hizo zinatakiwa kulipa fedha hizo kulingana na maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyetaka ziwalipe wakulima kwa kuwa taasisi za fedha zimeshakubali kutoa fedha.

“Kampuni ya Oram wameahidi leo kuwa wataanza kulipa, naombeni mfuatilie kwenye maeneo yenu," amesema.