VIDEO: Kampuni ya NMG, MCL zamlilia Ali Mufuruki

Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Leonard Mususa akitoa salamu za rambirambi wakati wa tukio la kuagwa kwa mwili wa mfanyabiashara maarufu, Ali MUfuruki jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Nation Media Group (NMG) zinazojishughulisha na masuala ya habari katika nchi za Afrika Mashariki na Kati zitakumbuka mchango uliotolewa na mfanyabiashara wa Tanzania, Ali Mufuruki.

Dar es Salaam. Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ya Kenya na Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Tanzania zitamkumbuka mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki kwa mchango wake katika kampuni hizo.

Mufuruki aliyefariki dunia Desemba 8, 2019 katika jiji la Johannesburg,  Afrika Kusini alishiriki kwa uwezo wake kuijenga MCL na waandishi wake ambao wengine  wamekwenda kuajiriwa maeneo mengine.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa wakati akitoa salamu za rambirambi za MCL na baadaye kusoma ujumbe wa mwenyekiti wa Bodi ya NMG, Wilfred Kiboro.

Mufuruki aliagwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo Jumanne Desemba 10, 2019 na watu mbalimbali wakiwemo mabalozi walipata fursa ya kutoa salamu zao za rambirambi.

Enzi za uhai wake, Mufuruki aliwahi kuwa mwenyekiti wa MCL, ambayo ni kampuni tanzu ya NMG inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mitandao yake ya kijamii ikiwamo MCL Digital.

Mususa amesema licha ya kuwa Mufuruki alikuwa na umri mdogo, lakini alikuwa akijifunza mengi kutoka kwake kutokana na uwezo aliokuwa nao.

"Yeye ndiye aliyejenga na yeye alisaidia kujenga sekta ya habari, wapo waandishi wengi wametoka Mwananchi na kwenda kuajiriwa kwingine,” amesema Mususa.

"Pale Mwananchi  ukiongea na kila mtu bado wanaheshimu mchango wake, alikuwa anaendelea kuchangia katika magazeti yetu kwa fikra chanya," amesema Mususa

Mwenyekiti huyo amesema,"Mwananchi tumesikitika sana kwa msiba huu, sijui tutapata mtu kama yeye ila kwa kuwa amewajenga wengi tutampata."

Akisoma ujumbe wa Kiboro, Mususa amesema NMG itamkumbuka Mufuruki kwa uwezo wake, kufanya kazi kwa kujituma, kuwafundisha wengine kifo chake ni pigo kubwa si kwa Tanzania pekee bali hata nje ya Tanzania.

Amesema Mufuruki ametoa mchango mkubwa kwa NMG kwani amechangia kwa sehemu kubwa na Mungu aijalie familia, ndugu na jamaa waliofikwa na msiba huo.

Mususa akiendelea kumzungumzia Mufuruki amesema alikuwa jasiri katika kufanya uamuzi wake na kujieleza kwenye mambo mbalimbali aliyokuwa anayaamini.

Mufuruki ambaye alikuwa anamiliki makampuni mbalimbali ya teknolojia na maduka makubwa amefariki akiwa na umri wa miaka 61.