Kampuni zatoa Sh120 milioni upasuaji wa moyo kwa watoto

Baadhi ya kina mama na watoto wao wanaotarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Muktasari:

Kampuni zaidi ya 20 zimetoa Sh120 milioni kwa ajili ya kuchangia upasuaji wa moyo kwa watoto 60 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Dar es Salaam. Kampuni zaidi ya 20 zimetoa Sh120 milioni kwa ajili ya kuchangia upasuaji wa moyo kwa watoto 60 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Mchango huo umetolewa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuunda kamati maalum kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa watoto hao.

Wwatoto 500 waliofanyiwa vipimo JKCI wanahitaji Sh1 bilioni ili kufanyiwa upasuaji.

Akikabidhi fedha hizo mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Charles Kimei amesema bado wanaendelea kukusanya  michango kwa ajili ya matibabu ya watoto hao ili watibiwe.

Dk Kimei amesema matendo yana nguvu kuliko maneno katika kuwasaidia watoto hao wanaohitaji msaada.

Makonda amewataka Watanzania kutoka katika utamaduni wa kusaidia watu wanaowafahamu pekee badala yake wawafikie na wenye uhitaji.

"Inauma sana ninapoona baba au mama anashindwa kumudu gharama za matibabu ya mwanaye, tuwasaidie watoto hawa," amesema Makonda.

Mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji, Veronika Lukas amesema hakujua ni wapi angepata fedha kwa ajili ya matibabu ya mwanaye.

"Nilipotajiwa gharama ya matibabu sikujua kama ningemudu, sina uwezo na mtoto pona yake ni upasuaji," amesema Veronika.