Kanisa Katoliki latoa mwongozo wa Pasaka

Padri wa shiri-ka la Ndugu Wafransisko Wakapuchini, Castor Ngowi akinawa miko-no kwa maji yenye klorini ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona baada ya kumaliza kuongoza misa ya Jumapili katika kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam. Picha ya Maktaba

Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku 11 kuanza maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka duniani, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa utaratibu wa jinsi ibada zitakavyoendeshwa katika wiki ya mwisho ili kuwakinga waumini na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19).

TEC wametoa utaratibu huo wakiunga mkono mwongozo uliotolewa na kanisa hilo duniani kwenda nchi mbalimbali unaoelekeza namna ibada za sikukuu ya Pasaka zinakazoanza Alhamisi Aprili 9, zinavyopaswa kuendeshwa katika kipindi ambacho dunia inapambana na ugonjwa huo wa homa kali ya mapafu.

Tangu ugonjwa huo ulipoibuka katika Jiji la Wuhan mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya watu 28,660 wameshapoteza maisha huku wengine zaidi ya 620,000 wakiwa na maambukizi katika nchi 199 duniani.

Kutokana na hatari ya virusi hivyo kuenea, tahadhari imetolewa ya kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kushikana mikono, kukumbatiana na baadhi ya nchi zimewazuia wananchi wake kutoka nyumbani ama kutenga muda maalum wa kwenda sehemu kwa ajili ya kufuata huduma muhimu.

Hadi sasa, Tanzania imetangaza watu 13 wenye maambukizi. Serikali imesema watu watakaoruhusiwa kutangaza habari za ugonjwa huo ni watatu-- Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali, lakini jana Zanzibar ilitangaza mgonjwa mwingine.

Hata hivyo, shughuli za dini hazijazuiwa na viongozi wametoa maelekezo ya jinsi ibada zinavyotakiwa ziendeshwe, ikiwa ni pamoja na kutoshikana mikono, kuweka maji ya kunawa au vitakasa mikono ili kuwakinga waumini wao na maambukizi.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima aliiambia Mwananchi jana kuwa utaratibu huo umetolewa kwa kanisa hilo duniani na utapaswa kutekelezwa na makanisa kwa kuzingatia hali katika nchi husika.

“Kuna mwongozo wa kimataifa uliotolewa ambao utategemea na sheria za nchi linapokwenda kutumika. Sisi hapa tunafuata sheria na taratibu za nchi zilizotolewa na waziri mkuu, waziri wa afya na msemaji mkuu wa serikali ambao mpaka sasa hawajazuia mikusanyiko ya ibada,” alisema Padri Kitima.

“Umetolewa mwongozo wa kimataifa. Sisi kama taifa tumeuridhia na utekelezaji wake utategemea uamuzi wa jimbo na Tanzania tuna majimbo 34. Lakini tunachopaswa kufanya ni huduma za kiroho zinazotolewa isiwe sababu ya kuambukiza corona.”

Mtendaji mkuu huyo wa TEC alisema mpaka sasa nchini kwa kuzingatia majimbo hayo ambayo utaratibu zaidi utakuwa ukitolewa na askofu wa jimbo husika, “kuna maeneo ambayo ni hatarishi na maeneo mengine hayana watu wengi sana. Tunajitahidi sana kuepuka mibanano”.

Mwongozo huo unaelekeza kuwa Alhamisi Kuu hakutakuwa na kuoshwa miguu wala maandamano ya Ekaristi takatifu hayatafanyika na badala yake sakramenti takatifu itahifadhiwa katika tabernako.

“Miguu haitaoshwa kabisa siku hiyo na wala kuabudu Ekaristi usiku haitakuwapo labda maeneo machache sana. Lengo ni kuepusha mikusanyiko ya muda mrefu,” alisema Padri Kitima.

Kuhusu Ijumaa Kuu, alisema hakutakuwa na utaratibu wa kubusu msalaba badala yake, “watainamia msalaba kwa mbali bila kuugusa, bila kuushika”.

Alisema maandamano mbalimbali ya sikukuu hiyo hayatakuwapo na utaratibu utafanyika kwa maaskofu katika majimbo yao kuhakikisha hakuna misongamano mikubwa. Alisema lengo ni kuwalinda waumini na maambukizi ya corona.

Mwongozo huo wa baraza hilo unaotokana na ule wa kimataifa umetolewa siku chache kupita tangu Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga kutoa utaratibu ulioanza kutekelezwa na kanisa hilo nchini.

Miongoni mwa taratibu hizo ni kusitisha kwa muda kuweka maji ya baraka ya kuchovya katika milango, Askofu Mkuu Nyaisonga akisema, “tutatakiwa kutumia maji ya baraka kadri tutakavyoelekezwa kijimbo”.

“Wakati wa kutakiana amani tusipeane mikono na waamini wafumbe mikono na kuinamiana kwa heshima. Waumini watakomunika kwa mikono tu, mapadri wazingatie hili wanapowakomunisha watu,” alisema.

Mwongozo mwingine ni kila muumini kutumia kitabu chake cha ibada. Wale wote wanaohesabu fedha za matoleo, watumie vitakasa mikono (sanitizers) kujisafisha.

Mwongozo mwingine ni utaratibu wa sakramenti ya kitubio, akisema Padri anayeungamisha na mwamini wasiangaliane uso kwa uso na kiti cha kitubio kisitumike bali maungamo yafanyike sehemu ya wazi.