Kanuni za uchaguzi serikali za mitaa zawaibua Mbowe, AG bungeni

Muktasari:

Wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema wamehoji kuhusu mchakato wa kutunga Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 huku wakitaka uchaguzi huo kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe amehoji iwapo ni sahihi kwa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 kuanza kutumika kabla ya  Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo kuziona.

Mbowe amehoji leo Alhamisi Septemba 5 2019, wakati alipopata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.

Amesema inawezekana watu wakaona mambo (uchaguzi) hayo ni mepesi lakini amani ya nchi itapotea ama kuathirika kama yasipowekwa sawa.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai amesema sheria ndogo na kanuni zinazotungwa zozote nchini ni lazima ziangaliwe Bungeni lakini vikao vinavyokaa kujadili mabadiliko ya sheria haviwezi kuwa mbadala ya Bunge.

Amesema kamati ya Sheria Ndogo haijawahi kuona wala kupitia kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Mheshimiwa Waziri atueleze katika utamaduni huo ambako tayari kanuni zimeshaingizwa kazini kamati ya Sheria Ndogo haikuzipitia kwa kisingizio wadau walipitia ni jambo hili ni sahihi,” amehoji Mwenyekiti huyo wa  Chadema

Akijibu swali hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Profesa Adelardus Kilangi amesema sheria ndogo zikishatayarishwa huwa zinapelekwa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uchambuzi.

Amesema baada ya uchambuzi, hurudishwa kwa waziri mhusika ambaye huchapisha katika Gazeti la Serikali halafu baada ya hapo hupelekwa katika kikao kinachofuata cha Bunge kwenye kamati ndogo ya sheria kwa ajili ya kuchambuliwa.

Amesema kimsingi sheria ndogo inatungwa chini ya sheria mama na kuna misingi inayofuatwa na kwamba mojawapo ya misingi hiyo ni isipingane na sheria mama.

Amesema baada ya kupelekwa bungeni kama kuna changamoto, kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo hutoa maelekezo na Serikali hurekebisha.

“Mheshimiwa mwenyekiti hakuna tatizo lolote katika eneo lolote,” amesema.

Katika maswali ya nyongeza, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema Katiba inasema Bunge linaweza kutunga sheria ya kuipa jukumu lolote Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Amesema pamoja na hilo, Nec haikuwa na jukumu la kusimamia kura ya maoni lakini Bunge lilitunga sheria ya kusimamia kura ya maoni.

“Kwanini Serikali imeogopa kuleta bungeni sheria ya kuipa mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa. Hiyo ingeondoa waziri kusimamia uchaguzi,” amehoji.

Mnyika amesema kanuni hazijazingatia maoni ya vyama vya siasa na wadau na kwamba tayari zimeshaanza kutumika vibaya kwa kuona wakuu wa  mikoa na wilaya ambao ni makada wa CCM kupewa majukumu ya kusimamia uchaguzi.

Amehoji kama kutakuwa na uchaguzi wa haki hapo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mwita Waitara amesema licha ya Serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria  lakini pia mbunge lina nafasi hiyo.

“Ungeleta marekebisho tungejali. Uchaguzi utasimamiwa na waziri mwenye dhamana (wa Tamisemi) utaratibu haujabadilishwa, sio lazima Serikali ichukue kila maoni,” amesema.

Waitara amesema maoni yakitolewa wataalam watakaa wanaangalia Katiba, sheria, miongozo mbalimbali na mambo ya kawaida.

Amesema kanuni hizo hazikuwapa dhamana wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya kusimamia uchaguzi.

“Usiogope uchaguzi utakuwa wa huru na haki. Tujipange tukutane kazini,” amesema Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga (CCM)