Kardinali Pengo awashangaa wanaomwita Rais Magufuli dikteta

Monday November 18 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Polycarp Kardinali Pengo  amewashangaa watu wanaomuita Rais wa Tanzania, John Magufuli dikteta na kueleza kuwa wanakosea.

Akizungumza leo Jumatatu Novemba 18, 2019 wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini na Mkuu wa mkoa wa Dar Paul Makonda, Kardinali Pengo amesema kumekuwa na watu wanaozungumza maneno ya kupotosha kuhusu rais Magufuli.

“Katika mitandao kumezuka maneno kwamba Rais wetu ni dikteta. Hivyo yale anayoyafanya anashughulikia kuendeleza vitu kuliko kuendeleza watu.”

“Wanaongelea juu ya kushughulikia vitu kuliko watu, ni watu gani hao hawajashughulikiwa wakati mambo mengi yanafanyika kwa ajili ya watu,” amesema Kardinali Pengo

Kiongozi huyo wa kiroho amesema, “Ni lugha ambayo kwa akili zangu za kizee siwezi kuelewa, utakuwa unamshughulikia mtu kiasi gani kama unamfanya mtoto wake na mjukuu wake waende shule.”

Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam amempongeza Makonda na kumtaja kuwa ni miongoni mwa wasaidizi bora wa Rais Magufuli.

Advertisement

“Nimefurahi, imenidhihirishia wewe ni kiongozi wa aina gani na tunamuomba Mungu atujalie viongozi wa aina yako wengi. Wewe (Makonda) ni mmoja kati ya wasaidizi bora wa Rais Magufuli.”

“Tunajiuliza baada ya Magufuli atakuwa nani ila mkiwepo wengi wa aina yako nisingekuwa na shaka ya kuwaza nani atafuata baada  yake,” amesema

Advertisement