Katiba Mpya hitaji muhimu la wananchi, si la kipaumbele

Sunday September 15 2019

 

By Anthony Mayunga, Mwanza

Mwaka 1991 Rais wa Awamu wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu mfumo wa vyama vya siasa unaofaa ikiongozwa na aliyekuwa Jaji mkuu Francis Nyalali.

Ripoti ya Jaji Nyalali ilionyesha kuwa ni alisimia 20 tu ya Watanzania walikuwa wanataka mfumo wa vyama vingi urejeshwe wakati asilimia 80 walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee.

Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alitoa hoja kuhusu takwimu hizo akisema ingawa asilimia 80 ya Watanzania bado wanataka mfumo wa chama kimoja uendelee, lakini ndani ya maelezo yao kumejaa shaka kwamba mfumo wa chama kimoja haufai kuendelea. Asilimia 80 ya Watanzania waliohojiwa walisema wanataka mfumo wa chama kimoja na asilimia 20 wakataka vyama vingi. Hivyo, Serikali iliamua wachache wapewe ndipo Tanzania ikaingia kwenye mfumo huo kwa kuwa lilikuwa hitaji wananchi na mabadiliko ya kidunia.

Mwaka 2012 Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba.

Tume ilifanya mikutano 1,942 katika maeneo mbalimbali ya nchi wakitumia njia shirikishi na kutengeneza rasimu ya Katiba ya wananchi kuhusu Tanzania waitakayo.

Baadaye rasimu hiyo ilipita katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo liliichakata na kuandaa Katiba Inayopendekezwa ambayo ilihitaji kura ya maoni ili kupata Katiba Mpya.

Advertisement

Hata hivyo, hatua hiyo haikufikiwa kwa wakati kwa kilichoelezwa ni nchi

kuingia katika Uchaguzi Mkuu ambao Rais aliyechaguliwa, John Magufuli alisema Katiba si kipaumbele chake, yeye anajenga nchi.

Hata hivyo, msimamo huo unaelezwa na wadau wa Katiba wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kushirikisha watu mbalimbali jijini Mwanza, kuwa si sahihi kwa kuwa Katiba Mpya ni hitaji la wananchi.

Dk James Jesse, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasisitiza kuwa Katiba Mpya ni muhimu kwa kuwa mbali na kuwa hitaji la Watanzania itaweka ulinzi wa mambo ambayo Rais anapambana nayo ili kila kiongozi anayekuja akute misingi fulani na kuzuia kila mtu kuja na mambo yake.

Dk Jesse ambaye ni mbobevu wa masuala ya Katiba, anasema Katiba ya sasa ya mwaka 1977 haijaweka Tume ya maadili ya viongozi, chombo ambacho ni muhimu kuwa kwenye sheria hiyo mama.

“Rais atapambana na ufisadi narushwa, ananunua ndege na kufanya mambo mengine makubwa, kwa Katiba tuliyonayo haijasaidia kwa kuwa hakuna sehemu inaweka chombo cha kuwabana watumishi kimaadili. Katiba Inayopendekezwa iliweka misingi hiyo na hilo ndilo hitaji la wananchi kwa sasa,” anasema.

Anasema Serikali inatakiwa kuanzisha mchakato wa Katiba kwa kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, maana nchi zote zilizoendelea zimeweka mambo muhimu kwenye Katiba na Rais wanayemchagua anabanwa na Katiba hiyo.

“Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitumia fedha nyingi za walipa kodi, kuacha kazi hiyo bila kufanyiwa kazi ni dhahiri kuwa hatupambani na matumizi mabaya ya fedha za umma. Kwa kuwa jambo hili lilianzishwa kwa maslahi ya umma ni vema likaendelea ili kuleta matokeo kusudiwa,” alibainisha.

Alisema kila Mtanzania anatakiwa kukumbushia Katiba na si suala la wachache na mashirika kama LHRC.

Na kuwa madaraka yanatoka kwa wananchi na ndiyo waliotaka mabadiliko ya Katiba ili watengeneze Tanzania mpya yenye umoja na inayoheshimu misingi ya haki ni budi wakapata walichokusudia

Kutokana na umuhimu, mwanasheria huyo, anaitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itekeleze majukumu yake kwa kutoa elimu ya uraia na kusambaza machapisho mbalimbali.

Msomi huyo wa sheria anaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Equality For Growthy Organization, Jane Magigita aliyesema Katiba zinazotokana na wananchi na viongozi wakaziheshimu husaidia kuweka nidhamu kwa viongozi wanaochaguliwa.

Anatolea mfano wa Kenya, kuwa Jaji David Malaga aliweza kufuta matokeo ya Rais si kwa nguvu zake bali kwa katiba yao,” anasema.

Magigita anazungumzia uhusiano wa katiba na amani ya nchi akisema nchi ambayo Tume ya Uchaguzi inakuwa huru na nguvu za kisheria, watu wanaingia kwenye uchaguzi wakiwa na imani kubwa kwa kuwa wana haki ya kuhoji matokeo yote na mamlaka zikaamua kwa kuwa anayechaguliwa anaelewa kuwa madaraka yanakuwa kwa wananchi.

Anasema hata ajenda ya wanawake 50 kwa 50 katika uongozi kufikia mwaka 2030 inatakiwa kuwa kwenye sheria mama ili isigeuke hisani kwa kila kiongozi anayeingia, ana anapokuwa amekwenda kinyume aonekane anaikanyaga Katiba aliyoapa kulinda na hivyo ahojiwe.

Mwanaharakati huyo anaibua hoja nyingine kuwa wanachama wa vyama vya siasa ni wachache ukilinganisha na Watanzania wasiokuwa kwenye vyama, lakini hawana haki ya kugombea nafasi yoyote mpaka wajiunge na vyama.

Hata hivyo, anasema pamoja na kunyimwa haki hiyo, anasema Katiba ya sasa inasema kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila mmoja.

Baada ya hoja hizo, William Mtwazi, mwanasheria kutoka LHRC anapendekeza namna ya kutoka katika mtanzuko huo, akisema wananchi wanatakiwa kuibua mchakato wa katiba ili uendelee kuwawezesha kutunga sheria nzuri zinazotoa usawa, haki, wajibu na wataokaokwenda kinyume wahojiwe.

“Licha ya nchi kupiga hatua kimaendeleo, kuna mambo ya msingi hayajapewa nguvu kama kaki za msingi, haki za binadamu na ndiyo maana kila kiongozi anafanya anavyoona inampendeza,” alisema.

Mmoja wa wanaharakati ambaye hakutaka jina litajwe alisema,” tunatakiwa kuiga Kenya mwaka 2008 baada ya machafuko waliunda timu ya watu tisa wakaanza kuamsha rasimu mbili zilizoleta mvutano na hatimaye mwaka 2010 wakapata Katiba iliyozinduliwa Agosti 27, 2010 na kuponya majeraha yao,” alisema.

Anasema katiba huleta muafaka wa kitaifa unapokosekana taifa linagawanyika na viongozi wanalazimika kutumia vyombo vya dola kama njia ya kunyamazisha watu. Watu wanaenda kwenye uchaguzi hawana imani na wanaosimamia kabla na baada ya uchaguzi, pia hakuna umoja wa kitaifa.

Anasisitiza umuhimu wa Katiba katika kujenga utawala bora akirejea hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa maendeleo ya vitu wakati watu ndani hawana uhuru wa kuzungumza hayana maana yoyote

“Katiba ya sasa imeweka mihimili mitatu, Bunge, Serikali na Mahakama lakini haijaanisha upi ni mhimili mkuu juu ya mingine, lakini kinachoonekana serikali imejipambanua kuwa kubwa. Inafanya itakavyo na hakuna anayehoji, haya mambo lazima yawe huru kwa kila chombo, ndipo tutafikia maendeleo ya kweli,” anasema.

Advertisement