Katibu CCK matatani akidaiwa kujifanya ofisa wa Takukuru, kuomba rushwa Sh50 milioni

Katibu mkuu wa Chama siasa cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi

Muktasari:

Katibu mkuu wa Chama siasa cha Kijamii (CCK) nchini Tanzania, Renatus Muabhi anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kujifanya mtumishi wa taasisi hiyo na kuomba rushwa ya Sh50 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Bharya Engeneering & Contracting Company Limited (Becco) iliopo Vingunguti Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Manraj Bharya.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania inamshikilia Katibu mkuu wa Chama siasa cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi akituhumiwa kujifanya mtumishi wa taasisi hiyo na kuomba rushwa ya Sh50 milioni.

Taarifa kwa umma ya Mkuu wa Takukuru mkoa wa Ilala, Dar es Salaam nchini Tanzania, Christopher Myava  aliyoitoa leo Alhamisi Desemba 12, 2019 imesema inamshikilia Muabhi kwa kosa la kujifanya mtumishi wa Serikali kutoka Takukutu na kuomba rushwa ya Sh50 milioni toka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Bharya Engeneering & Contracting Company Limited (Becco) iliopo Vingunguti Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Manraj Bharya.

“Uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba Renatus Muabhi dhumuni lake lilikuwa kuomba rushwa hiyo ili amsaidie Manraj Bharya katika tuhuma zake zilizokuwa zinamkabili Independent Power Tanzania Limited (IPTL),” amesema Myava

“Mtuhumiwa alikamatwa Desemba 10, 2019 majira ya jioni katika ofisi za kampuni ya Bharya Engeneering & Contracting Company Limited (Becco) akiwa amepokea fedha za mtego wa rushwa kiasi cha Sh1 milioni.”

Myava amesema uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

“Natoa rai kwa wananchi kujihadhari na matapeli wa aina hii na kujiepusha nao, na endapo wakibaini wahalifu wowote wa namna hii watoe taarifa Takukuru ili uchunguzi ufanyike na watuhumiwa waweze kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki,” amesema