Katibu mkuu Tamisemi atoa maelekezo ununuzi vifaa miradi ya afya

Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Dorothy Gwajima

Muktasari:

Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeziagiza kamati za ujenzi wa miradi ya afya na idara ya ununuzi katika halmashauri zote nchini kuwashirikisha wakuu wa idara za afya wakati wa manunuzi ya vifaa vya ukamilishaji wa majengo hayo.

Rorya. Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Dorothy Gwajima, ameziagiza kamati za ujenzi na idara ya ununuzi  kwenye miradi ya afya nchini, kushirikiana na wakuu wa idara za afya kununua vifaa vinavyohitajika kwaajili ya majengo yanayojengwa ili kuepuka gharama za ziada zinazojitokeza kutokana na ununuzi wa vifaa visivyotakiwa.

Dk Gwajima ametoa agizo hilo leo Novemba 4, 2019 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Rorya mkoani Mara, mradi ambao serikali imetoa jumla ya Sh1.5 bilioni kwaajili ya ujenzi wake

Amesema kuwa wamegundua kuwepo kwa ununuzi wa vifaa ambavyo haviendani na mahitaji ya kitaalam ya idara husika katika maneno mengi nchini kutokana na wataalam wa idara hizo kutokushirikishwa wakati wa manunuzi ya vifaa hivyo.

Amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha serikali kuingia gharama za ziada hasa wakati majengo hayo yakifikia hatua za mwisho za umaliziaji (Finishing) jambo ambalo lingeweza kuepukwa endapo wataalam hao wangeshirikishwa.

“Naziagiza halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanawashirikisha wataalam husika wakati wa ununuzi wa vifaa vya finishing ili kuepuka gharama zisizokuwa za msingi lengo ni kuokoa fedha na muda pia,” amesema Dk Gwajima.

Amesema kuwa wamegundua kuwa maeneo mengi maafisa manunuzi wamekuwa wakinunua vifaa bila kuwashirikisha wataalam husika hivyo kujikuta wananunua vifaa ambavyo haviendani na mahitaji husika ya jengo husika.

“Utakuta mtu wa manunuzi yeye anakimbilia kununua labda vigae bila kujua ni vya aina gani vinafaa kwa ajili ya maabara na mwisho wa siku hivyo vigae vinabomolewa na kulazimika kuingia gharama upya kununua vigae vinavyotakiwa wakati angeshirikishwa mtaalam wa idara husika hiyo hasara isingekuwepo,” amesema.

Amesema kuwa kabla ya kufanya manunuzi hayo ni lazima mkuu wa idara husika kusaini mahitaji yanayokwenda kununuliwa huku akisema kuwa watu wa manunuzi wamekuwa wakidai kuwa taratibu za manunuzi hazijasema mkuu wa idara husika kushirikishwa kwenye manunuzi jambo ambalo amesema kuwa si kweli kwa maelezo kuwa wakuu hao wa idara ndio wanaojua mahitaji halisi ya majengo yao.