Breaking News

Katibu wa CCM anayedaiwa kujinyonga azikwa kijijini kwao Tsaayo, Manyara

Friday December 6 2019

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Katibu wa CCM Tawi la Tsaayo Kata ya Arr, Wilayani Babati Mkoani Manyara, Nicodemu Panga anayedaiwa kujinyonga Desemba 2, 2019 kutokana na matatizo ya kifamilia, amezikwa jana.

Panga ambaye ameacha watoto watano, alifariki dunia kwa kujinyonga baada ya kukosana na mke wake.

Amezikwa jana Ijumaa Desemba 5, 2019 katika Kijiji cha Tsaayo.

Katibu wa CCM Wilayani Babati, Filbert Mdaki amesema kifo hicho kimewasikitisha na kimewaachia pengo na majonzi makubwa.

Mdaki amesema kwa mujibu wa ndugu wa marehemu chanzo cha kifo hicho cha Panga ni matatizo ya kifamilia, hata hivyo hawakuweka wazi.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai  Mkoani Manyara, Joshua Mwafulango amesema Panga alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kanga Desemba 2, mwaka huu.

Advertisement

Mwafulango alisema bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho licha ya ule wa awali kuonyesha ni matatizo ya kifamilia.

Mmoja wa majirani wa familia hiyo,  John Humay ameliambia Mwananchi kuwa Panga alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mke wake ambaye alikaa naye muda mrefu na kuzaa naye watoto sita ila mmoja alifariki dunia.

Hata hivyo, amesema Panga alitengana na mkewe, hadi umauti unamkuta ndugu walikuwa wakifanya jitihada za kuwasuluhisha kwa kuitisha vikao vya mazungumzo ya kuwarejesha pamoja.

“Maisha yake yalianza kuyumba hivi karibuni baada ya kuona anaishi bila mwenza wake ndipo akajinyonga kwa kutumia kanga na kufariki dunia na kisha kuzikwa,” amesema jirani huyo.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Aloyce Tsaxara alisema, “Kujiua siyo suluhisho la kumaliza matatizo ya dunia, ebu wafikirie wale unaowaacha, wengine wanasafiri hadi India kutafuta matibabu wewe unajinyonga kwa jambo lisilo na maana,” alisema Tsaxara.

Advertisement