TUME HURU: Kauli ya Dk Bashiru yawaibua wanasiasa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali kusema kwamba suala la Katiba mpya si la muda mfupi, viongozi wa vyama vya siasa wamemjia juu na kusema suala hilo halijaanza sasa na kwamba bado Watanzania wanahitaji Katiba mpya.

Wakizungumza na Mwananchi wameitaka Serikali kurejea mchakato wa Katiba mpya kwa sababu hiyo ni ajenda ya wananchi ambayo wamekuwa wakiidai kwa muda mrefu.

Viongozi hao wamesema jambo hilo likifanyika litaimarisha demokrasia nchini kwa kuruhusu kuundwa Tume huru ya uchaguzi hivyo kupunguza malalamiko katika mfumo wa uchaguzi.

Kauli za viongozi hao zimekuja ikiwa ni siku moja tangu Dk Bashiru aliposema kuwa wanaodai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi ni viongozi wanaotaka kuingia Ikulu ndani ya wiki moja.

Dk Bashiru alisema jambo hilo si la muda mfupi bali linachukua muda mrefu kwa sababu linapitia michakato tofauti. Alieleza kushangazwa na wanasiasa kupora ajenda hiyo ya wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Dk Bashiru alisema wanaodai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi ni viongozi wanaotaka kufika Ikulu “ndani ya wiki moja.”

Alisema wanaodai Tume huru wanapaswa kutambua kuwa suala hilo ni mchakato unaopaswa kupitia hatua tofauti.

Hata hivyo, wanasiasa wamepinga kauli hiyo wakieleza kuwa suala la Katiba mpya halijaanza sasa, bali lilianza miaka mingi ndiyo maana Serikali ya awamu ya nne ilianzisha mchakato kwa kuunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK), hata hivyo, Katiba haikupatikana.

Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema kauli hiyo inaonyesha jinsi kiongozi huyo asivyokuwa na kumbukumbu hata kwa maneno yake mwenyewe juu ya suala la Katiba mpya na umuhimu wake kwa Taifa.

“Nakumbuka Dk Bashiru aliwahi kuialika Serikali akasema ‘Katiba iliyopo sasa haiwezi kukidhi mahitaji kwa sababu iliandikwa wakati wa mfumo wa chama kimoja’. Yote hayo ameyasahau,” alisema Doyo.

Alisema anatambua suala la Katiba mpya linachukua muda lakini wangependa kuona mchakato unaanza ili kufikia malengo. Aliongeza kuwa tatizo ni kwamba Serikali haina utashi wa kisiasa wa kuwa na Katiba mpya.

“Tatizo ni kwamba Serikali haina dhamira ya kuwa na Katiba mpya na Rais John Magufuli aliwahi kusema kwamba Katiba mpya si kipaumbele chake, kwa hiyo nadhani Dk Bashiru ametembea kwenye maneno ya mwenyekiti wake,” alisema kiongozi huyo.

Doyo alisema Serikali haina budi kutengeneza katiba nyingine kwa sababu wananchi ambao ni wenye na serikali yao wameamua kuwa na katiba mpya ambayo itatengeneza mazingira ya usawa hasa kuwa na Tume huru ya uchaguzi.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe alisema watu kudai Katiba mpya ni jambo la kawaida na halina kipindi maalumu cha kufanya hivyo.

Rungwe alisema mchakato wa Katiba mpya ulikwama kwa sababu CCM wenyewe waliona kwamba itawashinda. Alisema mchakato uliopita uliwashinda wao wenyewe kwa sababu hawakuitaka Rasimu ya Warioba na hata Katiba Iliyopendekezwa.

“Tunataka Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi, ilishindikana wakati ule ndiyo maana bado tunadai mpaka leo kwa sababu ya umuhimu wake kwa Taifa hili.

“Kauli ya Dk Bashiru si sahihi, labda alikosa cha kusema. Sisi tuliokuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba tulitaka Katiba mpya lakini CCM walikwamisha hilo. Tunataka wawapatie wananchi Katiba mpya,” alisema Rungwe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha NLD, Oscar Makaidi alisema watu wanadai Katiba mpya si kwa manufaa yao binafsi bali Taifa kwa ujumla ili kuweka uwanja sawa wa ushindani na kulinda amani ya Taifa hili.

“Suala hili si letu tu, limezungumzwa na wengi, hata wastaafu wa CCM; Mzee Mkapa (Rais mstaafu) amelizungumza kwenye kitabu chake, Mzee Pius Msekwa aliwahi kulizungumzia, Mzee Joseph Butiku naye alilizungumzia,” alisema Makaidi.

Mwanasiasa huyo alisema wananchi wamedai Katiba mpya kwa muda mrefu sasa, hivyo, anashindwa kumwelewa Dk Bashiru anataka muda gani zaidi ili kuwapatia wananchi Katiba yao.

Makaidi alisisitiza kwamba mpaka sasa haja ya kuwa na Katiba mpya bado haijafa, alisema ni lazima kuwa na Katiba mpya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania na kulinda amani na usalama wa nchi.

Katibu Mkuu CUF, Khalifa Suleiman Khalifa alisema CCM hawana dhamira ya kuleta Katiba mpya, hivyo hata maneno ya Dk Bashiru ni ya kupuuzwa kwa sababu hayana jipya. “Kauli nyingine ni za kupuuzwa tu, kwani amezungumza mambo mangapi ya ovyo? Siyo yeye aliyemwambia Suleimani Jafo kwamba wapinzani wakishinda atamfukuza kazi? Siyo yeye aliyesema alimpigia Msajili wa vyama vya siasa na kumwambia avidhibiti vyama vya upinzani?” Alihoji kiongozi huyo wa CUF.

Khalifa alisema Katiba mpya ni lazima na Serikali lazima ifanye hivyo, kama si Serikali hii basi zinazokuja. Alisema Katiba mpya ikipatikana, hali ya siasa itaimarika nchini ikiwemo maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa alisema Dk Bashiru ana haki ya kukataa Katiba mpya na Tume huru kwa sababu si yule wa zamani anayemfahamu kwa kutetea wanyonge.

Alisema tatizo lipo kwao kama wapinzani kwa sababu mpaka sasa hawajakaa pamoja kupanga mikakati, kila mmoja anakaa peke yake kumkabili CCM. Alisema hawataweza kuishinda CCM kama kila chama kitasimama peke yake.

“Wao (CCM) hawana haja na chochote kati ya Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi, tatizo lipo kwetu wapinzani. Mpaka sasa imebaki miezi minane ya uchaguzi mkuu lakini hatujafikiria kukaa pamoja, kila chama kimesimama peke yake. Hatuwezi,” alisema.

Alisema miaka ya nyuma walikaa pamoja na kutengeneza rasimu ya Katiba mpya na kumkabidhi aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na hapo ndipo mchakato wa Katiba mpya ukaanza baada ya Serikali kuibeba hoja yao.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema hakuna aasiyetambua umuhimu wa Katiba mpya na kwamba maneno ya Dk Bashiru ni kutaka kuizima hoja ambayo imekuwepo muda mrefu.

Alisema ili kufanikisha suala la Katiba mpya, Watanzania hawana budi kutumia nafasi zao kuidai. Amesema serikali haitaki kuandika Katiba mpya lakini wananchi wanataka, hivyo, lazima serikali itekeleze.

“Mabadiliko yoyote ya mfumo ni magumu lakini tusikatishwe tamaa na kauli za viongozi hawa. Tuendelee kudai katiba mpya kwa sababu ni haki yetu wananchi,” amesema kiongozi huyo wa ACT Wazalendo.

Naye, mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema chama hicho kitatoa kauli rasmi kuhusu jambo hilo.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania kuwa wamoja katika kupigania Tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya ili kujenga demokrasia imara katika Taifa hili na kuwafanya wananchi waishi kwa amani na furaha.

“Hii ni ajenda ni ya wananchi kwa muda mrefu, kwa hiyo tutaendelea kudai Tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya,” alisema mkurugenzi huyo wa Chadema.