UCHAGUZI MKUU 2020: Kauli ya Magufuli bado mjadala kwa wapinzani

Moshi. Kauli ya mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuwa upinzani umebadilika na una mbinu za wazi na za siri za ushindi, imewaibua viongozi wa upande huo wakisema kuimarika huko kunamaanisha hatua zichukuliwe kurekebisha uchaguzi mkuu.

Rais Magufuli aliwaambia viongozi wa CCM wa ngazi ya wilaya na mikoa juzi kuwa upinzani uliokuwepo miaka michache iliyopita, si uliopo sasa kwa kuwa umebadilika na una mbinu nyingi za ushindi na hivyo kuwataka kutobweteka hata kama chama hicho tawala kilipata ushindi wa asilimia 99 katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Lakini kauli hiyo imewafanya viongozi wa upinzani wamueleze Rais kuwa anapaswa kuweka sawa mazingira ya uchaguzi ili uwe wa amani, huru na wa haki.

Viongozi waliozungumza na Mwananchi ni James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema (TLP), Renatus Muhabi (CCK), Andrea Bomani (UDP) na John Shibuda wa Baraza la Vyama vya Siasa ambao walisema kauli ya Rais imetokana na kuona ukweli wa kuimarika kwa upinzani na hivyo kuna haja ya kuwa na mazingira sawa ya uchaguzi.

Mbatia, ambaye ni mbunge wa Vunjo, alimsihi Rais Magufuli kutambua kuwa upinzani upo kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, hivyo aone umuhimu wa kuijenga Tanzania pamoja badala ya kuwaona wapinzani kuwa ni maadui.

Mwenyekiti huyo alisema ni jambo la hatari kuingia katika uchaguzi mkuu wa 2020 wakati kuna walakini katika umoja wa kitaifa na akashauri kila mmoja atambue Tanzania kwanza, vyama vinakuja baadaye.

“Rais na Watanzania ni lazima wafahamu kuwa amani ni tunda la haki. Ili amani itamalaki katika uchaguzi mkuu huu wa Oktoba ni lazima kuwe na haki sawa ya siasa na ionekane kweli haki inatendeka,” alisema.

Mbatia alimsihi Rais na makada wa CCM wasiwaone maadui Watanzania wanaoitakia mema Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 na kuwapa majina, badala yake watambue wanaipigania Tanzania.

Naye Mrema alisema kauli ya Rais Magufuli inatokana na aliyoyaona katika chaguzi za nyuma, chaguzi ndogo na uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Ameona maeneo CCM ilipojikwaa na wapinzani walipopatia. Kwa hiyo ni tahadhari nzuri kwamba wasibweteke uchaguzi ni uchaguzi chochote kinaweza kutokea,” alisema Mrema.

“Wasifikiri kwamba mambo yanaweza kuwa bwerere kila siku. Ni baba anafunda watoto wake na usisahau ana vyombo ambavyo vinampa taarifa na ni lazima kuna taarifa wamempa juu ya kuimarika kwa upinzani.”

Kwa upande wake, Bomani ambaye ni kaimu katibu mwenezi wa UDP, alimtaka Rais Magufuli kuandaa mazingira bora ya uchaguzi na yasijengwe mazingira ya kuibeba CCM na vyama washirika.

Wosia wa Baraza la vyama vya siasa

Lakini Shibuda alisema kwa kuwa Rais ndio jemedari mkuu wa kuongoza fikra za chama chake, ni haki yake kutoa tahadhari na kuwaanda viongozi, wanachama na wafuasi wake.

“Rais Magufuli aliposema anataka vyama vya upinzani vife ikifika 2020 ilikuwa ni vita ya kisaikolojia na vita ya kisaikolojia na ana haki ya kuwa propagandist (mtu wa propaganda),” alisema Shibuda.

“Yeye si kafara la kushindanisha, yeye si kafara la kukweza chama chochote kama ambavyo (klabu ya soka) Yanga si kafara la kukweza ushindi wa CCM, vivyo hivyo CCM si kafara la kushindanisha ushindi wa upinzani,” alisema Shibuda, mahiri wa lugha anayejulikana kwa kutumia misemo, misamiati na nahau anapoelezea jambo.

“Rais Magufuli asitarajiwe na chama chochote kama msaada wa kifikra na wa kisaikolojia wa kukweza chama kingine. Kwa hali hiyo vyama vyote vya siasa vielewe vinakwenda kuingia katika uchaguzi kushindania imani.

“Kila chama kama kweli kina sauti ya rufaa basi kijiandae kwa mbinu bora ili kuteka imani na hisia za wapigakura. Kila chama kije na tiba mbadala itakayokubalika kwa wananchi ili waone CCM hapana.”

Mwaka 2015 CCM ilikabiliana na ushindani mkubwa tangu kurejeshwa kwa vyama vya upinzani mwaka 1992 na ilishinda kwa chini ya asilimia 60 katika uchaguzi wa Rais.

Magufuli alipata kura milioni 8.8 na mpinzani wake, Edward Lowassa wa Chadema na ambaye aliungwa mkono na vyama vingine vitatu, alipata kura milioni 6.07 ikiwa ni mara ya kwanza kwa upinzani kuvuka kura milioni 5.