Kauli ya Magufuli kuhusu uchaguzi mkuu kuwa huru mjadala mtandaoni

Muktasari:

Watu wa kada mbalimbali mwahoji utekelezaji wa kauli ya Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyesema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa huru na wa haki.

Dar es Salaam. Watu wa kada mbalimbali wamehoji utekelezaji wa kauli ya Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyesema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa huru na wa haki.

Baadhi ya waliotoa maoni yao katika mitandao mbalimbali ya kijamii ya Mwananchi wamerejea hali ilivyokuwa katika chaguzi ndogo zilizofanyika kuanzia mwaka 2017, kueleza kuwa ni vigumu kuwa huru na haki kwa kuwa katika chaguzi hizo zaidi ya 10 malalamiko, kasoro zilikuwa nyingi.

Magufuli alitoa kauli hiyo jana Jumanne Januari 21, 2020 katika hafla ya chakula cha jioni aliyowaandalia mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema shughuli ya uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi ya kidemokrasia kama Tanzania, hivyo Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya amani.

Wakizungumzia kauli hiyo, Zezeta_Lumumba amesema, “itakuwa ngumu sana kuamini hili. Imezuiwa mikutano ya kisiasa, Serikali za mitaa tumeona walichofanyiwa wapinzani, kifupi tunaelekea kuangukia pua kisiasa.”

Kwa upande wake  Beberu mweusi @Bonimawalla amesema, “tumeyaona kwenye Serikali za mitaa juzi uchaguzi ulikuwa huru sana na wapinzani wote hawajui kusoma na kuandika kasoro wa CCM tu.”

The OoompaLoompa @Ooompa amesema, “jamaa walicheza rafu ya kificho, nao wakachezewa rafu ya wazi watie akili. Achana na hayo bwana tugange yajayo. Uchaguzi utakua safi kabisa, labda hawa wapinzani wapenda waamue kuanzisha chokochoko.”

Naye Wb35t @BestHope7 alijikita kuzungumzia tume ya uchaguzi, “uhuru na haki haviwezi kwenda sambamba na tume ya uchaguzi ambayo wajumbe wake wanateuliwa na rais. Uhuru na haki vinakwenda sambamba na tume huru ya uchaguzi, wagombea wote kupewa haki sawa za kujinadi kwa wananchi na jeshi la polisi kuachana na siasa na kufanya kazi ya kusimamia usalama tu.”

 MK Ultra @MajesticIX  amesema, “habari hii haikutakiwa hata kuandikwa. Hakuna uchaguzi wa amani, huru na haki bila katiba mpya, bila tume ya uchaguzi.”

Naye Goodluck Mgeni amesema, “sioni uchaguzi huru na wa haki..., hamtakubali kuunda tume huru kwa sababu itakuwa sawa na kujichimbia kaburi wenyewe. Muda ni mwalimu mzuri, kadri miezi inavyozidi kusogea ndiyo ukweli wa maneno  unavyojidhihirisha. Dalili za awali zilishatuonyesha kuwa tuendako sio kwema.”

Kwa upande wake Oswald S Mayani amesema, “uchaguzi gani? Huu wa wagombea wa chama fulani kupita bila kupingwa?”

“Watanzania hatujasahau  yaliyotokea uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania, tuna kumbukumbu nzuri sana na yeye kama analisema hilo kwa haki basi kabla ya uchaguzi nchi yetu iwe na tume huru ya uchaguzi na wakurugenzi waondolewe kuwa wasimamizi wa uchaguzi, hapo ndio tutauona mwanga na viashiria vya kile akisemacho.”