VIDEO: Keissy ataka Nec ipange upya majimbo ya uchaguzi

Mbunge wa Nkasi Ali Keissy akichangia mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Nkasi Kaskazini Nchini Tanzania (CCM), Alli Keissy amelalamikia utofauti wa ukubwa wa majimbo nchini na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuangalia na kuyapanga upya.

Dodoma. Mbunge wa Nkasi Kaskazini Nchini Tanzania (CCM), Alli Keissy ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kupitia na kuyapanga upya majimbo nchini ili kuondoa tofauti ya ukubwa wa maeneo.

Akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mikoa (Tamisemi) kwa mwaka 2020/2021 leo Alhamisi Aprili 9, 2020 Keissy amesema halmashauri zimegawanya kisiasa.

Amesema kuna jimbo lina kata sita na kuna majimbo mengine yana kata kati ya 30 hadi 40 na kwamba inapokuja suala la kugawa fedha hawezekani kugawa kwa usawa.

“Halmashauri zipo kisiasa, kuna jimbo lina kata nane. Haiwezekani mheshimiwa Jafo (Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo) kugawa sawa fedha za kumalizia maboma sawa sawa,”amesema.

“Ni lazima tufuate idadi ya kata, hatuwezi kugawa kwa majimbo. Leo wanataka kupewa tena fedha kisiasa. Kule kwangu kata za Kabwe na Korongo ni sawa na majimbo mengine.”

Vilevile, Keissy amesema kuna baadhi ya wabunge wamelalamikia kuhusiana na posho lakini iliwahi kutamkwa bungeni kuwa madiwani walipwe kufuatana na makusanyo yao.

“Kama kuna halmashauri haiwezi kukusanya hata asilimia 80 ya mapato haifai kuwepo, waje wakurugenzi wajieleze hapa,”amesema.

Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameungana na Keissy kwa kuitaka Tamisemi kuangalia namna wanavyoweza kugawa fedha hizo kulingana na ukubwa wa majimbo.

“Hiyo ya kugawa fedha sawa sawa ni kweli linatakiwa kuangaliwa. Kuna jimbo lina kata 36 Sh140milioni lakini kuna jimbo lina kata 10 linapewa kiasi hicho hicho cha fedha na kila kata kuna maboma ambayo hajamalizika, haitakuwa sawasawa pengine kuangalia uhitaji wa watu ama kila kata,”amesema.