Advertisement

Kenyatta ataka mabadiliko ya katiba

Tuesday October 20 2020
kenyatttapic

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Kisii, Kenya (AFP). Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta leo Jumanne ameshauri kufanyika kwa mabadiliko ya katiba kwa ajili ya kuondoa tatizo la kujirudia kwa vurugu wakati wa uchaguzi, suala moto ambalo limegawanya wanasiasa.

Ushauri wa Kenyatta umekuja kabla ya ripoti inayosubiriwa kwa hamu kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa ambayo inatarajiwa kukabidhiwa siku zijazo, baada ya miaka kadhaa ya kupata maoni ya wananchi, muda ambao viongozi waliutumia kuzunguka kutaka taifa liunge mkono mchakato huo.

Mpango huo wa Building Bridges Initiative (BBI)-- au jitihada za kujenga madaraja-- ulikuja baada ya Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kulishangaza taifa mwaka 2018 waliposhikana mikono na kuahidi kuendeleza umoja baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017 kusababisha vurugu zilizoua zaidi ya watu 90.

"Hoja... inayotaka maridhiano ya kikatiba ni hii hapa: tunawezaje kutatua hali ya mshindi kuchukua kila kitu katika mukhtadha wa ushindani wa kisiasa kama inavyotakiwa na utamaduni wa kidemokrasia?" Kenyatta alisema wakati akihutubia wananchi katika sikukuu ya kitaifa ya kusherehekea mashujaa wa nchi hiyo.

"Hoja hii ya 'sisi' dhidi ya 'wao' lazima ifikie mwisho."

 'Kuzingatia tofauti zetu'

Advertisement

Kenya, ambayo ina watu wa makabila tofauti, kwa muda mrefu imeathiriwa na vurugu zinazotokana na tofauti za kikabila kila wakati wa uchaguzi, hasa uchaguzi wa mwaka 2007 wakati zaidi ya watu 1,100 walipouawa.

Uchaguzi huo ulisababisha kuundwa kwa serikali ya umoja, ambayo Odinga alikuwa waziri mkuu, na baadaye kuandikwa kwa katiba mpya mwaka 2010.

Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka 2017 ulikuwa na vurugu tena, baada ya Odinga kudai kulikuwa na mchezo mchafu na Mahakama Kuu kuamua urudiwe. Kenyatta alishinda katika uchaguzi wa marudio.

"Kwa kweli itakuwa janga kama tutakuwa hatujatatua tatizo hili wakati wa uchaguzi unaofuata," alisema Kenyatta.

"Hatuwezi kuwa na katiba ambayo itajali tofauti zetu kama binadamu?"

Mchakato wa BBI, na ukaribu wa Kenyatta na Odinga, umeibua mzozo huku naibu rais, William Ruto akidai kuwa wawili hao wanataka kuanzisha cheo cha waziri mkuu kwa ajili ya Kenyatta, ambaye haruhusiwi kugombea urais kwa kipindi cha tatu wakati wa uchaguzi ujao mwaka 2022.

"Msiupe ushauri wangu tafsiri ya kutaka kuanzisha vyeo kwa ajili ya watu," alisema Kenyatta.

Mzozo huo umeibua maswali kuhusu ahadi ya Kenyatta kuwa atamuunga mkono Ruto katika uchaguzi ujao, huku Odinga akionekana kama ataibuka mshindi.

 

Advertisement