Kesi ya Shamim, mumewe yasubiri majibu ya mkemia mkuu wa Serikali

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkadinda  na mkewe, Shamim Mwasha umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado wanasubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kukamilisha upelelezi.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkadinda  na mkewe, Shamim Mwasha umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado wanasubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kukamilisha upelelezi.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameeleza hayo leo Ijumaa Septemba 13, 2019 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo,  Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na bado wanafuatilia majibu kwa mkemia mkuu wa Serikali  na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine.

Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha gramu 232.70 za dawa za kulevya aina ya Heroin. Mbele ya Hakimu Mkazi mfawidhi Kelvin Mahina.

Inadaiwa kuwa Mei Mosi, 2019 kwa pamoja washtakiwa hao wakiwa maeneo ya Mbezi Beach walisafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 232.70 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa  kisheria.

SOMA ZAIDI