Kesi ya Zitto uteuzi wa CAG yaanza kutajwa

Muktasari:

Mahakama Kuu masjala Kuu Dar es Salaam imeanza  usikilizaji wa awali wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kuhusu uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu masjala Kuu Dar es Salaam imeanza  usikilizaji wa awali wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kuhusu uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

Kesi hiyo imeanza kutajwa mahakamani hapo leo Jumanne Januari 28, 2020  kwa ajili ya kuangalia taratibu za awali za mwenendo wa kesi hiyo ambazo ni pamoja na pande husika kukabidhiana nyaraka zinazohusu kesi hiyo, kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa chama hicho amefungua kesi hiyo dhidi ya Rais wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kichele na CAG  mstaafu, Profesa Mussa Assad.

Katika kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2019, Zitto anawakilishwa na wakili Nyaronyo Kicheere, anapinga Sheria ya Ukaguzi ya Taifa namba 11 ya mwaka 2008 inayoweka vipindi viwili vya mtu kushika wadhifa wa CAG.

Pia, anapinga uamuzi wa Profesa  Assad  kuondolewa katika wadhifa huo, akidai ameondolewa kabla ya muda wake wa utumishi kwa mujibu wa katiba.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu Jaji Lameck Mlacha (kiongozi wa jopo), Jaji  Benhajj Masoud na Jaji Juliana Masabo.

Waidaiwa ambao ni Rais, AG na CAG Kichere akiwakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali wanne, wakiongozwa na naibu Wakili Mkuu wa Serikali (DSG), Gabriel Malata na Profesa Assad anawakilishwa na jopo la mawakili wawili linaoongozwa na Ambros Mkwera, wameomba muda wa siku 14 kuwasilisha majibu.

“Waheshimiwa majaji, kwanza tunakiri kwamba tumepokea maombi haya yaliyoko hapa mahakamani, Januari 23, 2020.”

“Pili tunakusudia ku-contest (kupinga) maombi haya kwa ku-file (kuwasilisha) reply (majibu ya hoja) na counter affidavit (kiapo kinzani) chini ya kanuni ya 6 ya kanuni za uendeshaji wa mashauri ya haki za Binadamu. Tunakusudia ku-file majibu yetu ndani ya siku 14 zilizotajwa kwenye hiyo kanuni,” amesema  Malata.

Malata amefafanua kuwa kwa siku hizo  wanapaswa kuwasilisha mahakamani majibu yao.

Wakili Mkwera kwa niaba ya Profesa Assad naye amesema mteja wake anakusudia kuwasilisha kiapo kinzani dhidi ya hoja za mdai, na hivyo naye akaomba muda wa siku 14.

Mahakama imekubaliana na maombi ya mawakili hao na kuamuru kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao, kwa muda huo waliouomba.

Jaji Mlacha ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 18, 2020 itakapotajwa tena.