Kesi ya habari za uchochezi yaendelea kumsubiri Lissu

Muktasari:

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 24 kwa kuwa mshtakiwa Tundu Lissu yuko nje ya nchi kwenye matibabu

Dar es Salaam. Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wenzake watatu imeshindwa kuendelea kutokana na mbunge huyo kuwa kwenye matibabu nje ya nchi.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka amedai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji lakini mshtakiwa bado hajarejea nchini nakuomba tarehe nyingine.

"Shauri hili ni kwaajili ya kuendelea na usikilizwaji, mshtakiwa bado yuko kwenye matibabu nje ya nchi tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Wakili Nguka.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji kutoka Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.