Kesi ya madai chanzo ndege ya Air Tanzania kuzuiwa Afrika Kusini

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imezuia ndege ya Air Tanzania kuondoka nchini humo  kuanzia jana Jumamosi Agosti 24, 2019 kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Hermanus Steyn.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imezuia ndege ya Air Tanzania kuondoka nchini humo  kuanzia jana Jumamosi Agosti 24, 2019 kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Hermanus Steyn.

Steyn,  raia wa Afrika Kusini anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Agosti 25, 2019 na msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji nchini (TBC).

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 imeshikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg baada ya kufanya safari kadhaa tangu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lianze kufufua ruti zake za nje ya nchi.

Katika maelezo yake Dk Abbas amesema Steyn aliridhia mali hizo kutaifishwa lakini hoja ikaja alipwe fidia kiasi gani.

“Ndege zetu zipo salama kwa maana ya ndege sita ambazo Air Tanzania kwa sasa inaziendesha isipokuwa hii moja ambayo tumetoa taarifa kuwa imezuiwa kwa ajili ya kesi.”

“Watu wanahusisha jambo hili na madeni ya zamani kwenye shirika  kati ya Air Tanzania na Shirika la ndege Afrika ya Kusini. Niseme tu kuwa hii kesi haihusiani kabisa na hilo,” amesema Dk Abbas.

Ameongeza, “Alikuwa (Steyn) na mashamba, mifugo na mali nyingi kwa hiyo Serikali kwa wakati huo ikaona ni sahihi hizi mali zitaifishwe kwa hiyo ukitaka kuchimbua mgogoro huu asili yake unatoka miaka ya 1980.”

Amesema ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, miaka ya 2000 akalipwa na kuna kiasi kilichobaki ambacho mhusika amefungua kesi akitaka amaliziwe kulipwa.

“Ukiangalia awamu zote (za uongozi) kulikuwa na makubaliano, ukiangalia hatua za kimahakama wanakubaliana lakini malipo hayakufanywa lakini yalikuja kufanyika katika awamu ya nne,” amesema Dk Abbas.

Dk Abbas amesema mdai  huyo amekwenda Afrika Kusini kwa taratibu za mahakama, akibainisha kuwa zipo nchi ambazo mtu anaruhusiwa kuiomba hukumu ya nchi nyingine itekelezwe kwenye nchi aliyopo, akisisitiza kuwa ni  taratibu za kawaida kwenye sheria.

“Sisi tunaheshimu utawala wa sheria kwa sababu ni mfumo wa kawaida. Sheria itafuata mkondo wake, ukisoma ile hukumu inaturuhusu kuipinga.”

“Nafikiri  wanasheria wetu wataichambua na wataona hatua gani za kuchukua lakini ni mfumo wa kisheria ambao Serikali tunaufuata na tunauheshimu. Tunawahakikishia Watanzania kuwa tunasimamia maslahi ya Taifa,  ndege yetu itarudi na itaendelea na shughuli zake za kawaida,” amesema Dk Abbas.

Amesema kesi ya msingi haijasikilizwa kwa sababu anayedai fidia  ametumia sheria za Afrika Kusini kuomba kutekeleza hukumu ya nchi nyingine.

“Kesi ya msingi ya kiasi kilichobaki kwamba tukilipe haikusikilizwa, yeye aliomba maombi madogo ambayo pia yana sehemu mbili,  kusikilizwa wote (Serikali ya Tanzania na mdai) na mahakama au kusikilizwa yeye mwenyewe kama alivyofanya,” amesema Dk Abbas.

Kushikiliwa kwa ndege hiyo kunarejesha kumbukumbu ya ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 iliyozuiwa nchini Canada mwaka 2017 kutokana na madai ya Sh87.3 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi.