Kesi ya ukomo wa urais sasa mpaka mwakani

Friday November 22 2019

 

By James Magai, Mwananchi

Dar es Salaam. Kesi ya ukomo wa urais, iliyofunguliwa na mwananchi mmoja, Patrick Dezydelius Mgoya, imerushwa mpaka mwakani kutokana na kuwepo kwa maombi mengine ya kuunganishwa katika kesi hiyo.

Maombi hayo namba 55, ya mwaka 2019 yamewasilishwa mahakamani hapo na Mhina Shengena, akiomba kuunganishwa katika kesi hiyo upande wa mdai, ambayo yalitajwa jana kwa mara ya kwanza.

Kutokana na maombi hayo, leo Ijumaa, Novemba 22, 2019, mahakama hiyo imeshindwa kupanga tarehe ya kusikiliza pingamizi la awali la Serikali dhidi ya kesi hiyo, ikisema kuwa mpaka ikamilishe usikilizwaji wa maombi hayo.

Mahakama imepanga kuyasikiliza maombi hayo Desemba 12, mwaka huu na ikapanga kesi ya msingi itajwe Februari 10,2020.

Kesi hiyo namba 19 ya mwaka 2019 imefunguliwa na mwananchi mmoja anayejitambulisha kama mkulima, Patrick Dezydelius Mgoya, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mgoya anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya Ibara ya 40(2) ya Katiba ya Nchi inayoweka ukomo wa mtu kuchaguliwa kuwa rais.

Advertisement

Kwa mujibu wa ibara hiyo mtu hataweza kuchaguliwa kuwa rais wa Tanznaia kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka  mitano mitano tu yaani miaka 10.

Mgoya anadai kuwa masharti ya ukomo yanayowekwa chini ya ibara hiyo yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria  chini ya Ibara ya 13, 21 na 22(2).

Hata hivyo Serikali kupitia kwa AG tayari imeshamwekea pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na mambo mengine ikidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na kwamba kesi hiyo ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Wakati maombi hayo yalipotajwa, mjibu maombi wa kwanza, Mkulima Mgoya aliieleza mahakama kuwa hana pingamizi, lakini mjibu maombi wa pili, AG, kupitia kwa Wakili wa Serikali, Yohana Marko, aliomba wapewe siku 14 ili wawasilishe kiapo kinzani.

Mahakama ilikubaliana na maombi hayo baada ya Mkulima kusema kuwa hana pingamizi.

Hivyo Jaji Dk. Eliezer Feleshi alimwamuru AG kuwasilisha kiapo chake kinzani Desemba 5 na akapanga maombi hayo yasikilizwe Desemba 12, mwaka huu, saa nane mchana.

Kuhusu kesi ya msingi Jaji Feleshi alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa maombi hayo ya Shengena, hawawezi kupanga tarehe ya usikilizwaji wa pingamizi la Serikali, kwani haliwezi kusikilizwa bila maombi hayo kukamilika.

Baada ya maelezo hayo, wakili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), ambacho nacho kimeshaunganishwa katika kesi hiyo kama mdaawa mwenye maslahi, Daimu Halfani aliomba wapewe nakala ya hati ya maombi ya shauri la msingi na muda wa kuwasilisha kiapo chao kinzani.

“Amri ya mahakama. Shauri hili (la msingi) litatajwa Februari 10, 2020, saa tatu asubuhi na TLS wapewe nakala ya hati ya madai na wawasilishe kiapo kinzani kabla au Desemba 5, mwaka huu.”, alisema Jaji Feleshi.

Mbali ya TLS, Chama cha Alliance for Change and Transparency (Chama cha ACT- Wazalendo) nacho tayari kimeshaunganishwa katika kesi hiyo kama mdaawa mwenye maslahi.

Advertisement