Kibatala, wenzake wakwamisha kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

Mawakili wa upande wa utetezi unaoongozwa na Peter Kibatala umekwamisha kesi ya viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kutokana na kutokufika mahakamani.

Dar es Salaam. Kesi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe imeshindwa kuendelea kwa kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa utetezi kwa sababu mawakili wao hawakuwepo.

Mawakili hao ni; Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari na Hekima Mwasipu.

Katika kesi hiyo iliyokuwa iendelee leo Jumatano Novemba 13, 2019 katika Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam ambapo Mbowe alikuwa anapaswa kuendelea kujitetea kwa upande wa mashtaka kumhoji kuhusiana na ushahidi alioutoa mahakamani hapo.

Kufuatia hali hiyo, wakili wa utetezi, Dickson Matata ameieleza Mahakama kuwa anawakilisha mawakili Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari na Hekima Mwasipu wanaowatetea washtakiwa hao.

Matata amedai Kibatala na Profesa Safari hawakufika mahakamani hapo kwa sababu wapo kwenye kesi Mahakama Kuu ambapo zinasikilizwa Novemba 13 na 14, 2019.

Amesema Mwasipu hakufika mahakamani hapo kwa kuwa alihudhuria kesi katika Mahakama ya Wilaya Kilombero mkoani Morogoro leo Jumatano Novemba 13 na Novemba 14, 2019 atahudhuria katika kesi inayomkabili Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga na wenzake.

Matata baada ya kueleza hayo ameiomba Mahakama kuiahirisha kesi hiyo na kuomba iendelee kusikilizwa Novemba 26 hadi 29, 2019.

Kwa upande wake, wakili Nchimbi, alipinga ombi la kesi hiyo kuahirishwa kwa maelezo kuwa hakuna sababu za msingi zilizotolewa na upande wa utetezi kuahirisha kesi pia hawakutoa uthibitisho wowote ikiwemo samasi kuonesha kama ni kweli wapo Mahakama Kuu.

Hakimu Simba alisema kwa kutumia busara za Mahakama  hatoisikiliza Kesi hiyo Novemba 13 na 14 ila kwa kuwa Novemba 15 hakujaelezwa hao mawakili watakuwa wapi hivyo wajulishwe mapema na kwamba kesi itaendelea kusikilizwa tarehe hiyo saa 3 asibuhi.

Katika kesi hiyo Mbowe na wenzake wanaokabiliwa na  mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, manaibu Katibu Wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu. 

Pia, wabunge wa chama hicho, John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Esther Bulaya (Bunda Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).