Kibano kwa wasio na elimu ya uandishi

Dar es Salaam. Wakati Idara ya Habari Maelezo ya Zanzibar na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) zikipiga marufuku vyombo vya habari kuajiri wafanyakazi wasio na elimu ya masuala ya habari na utangazaji, wadau wa sekta ya habari wamesema suala hilo linatakiwa kuangaliwa kwa kina ili lisiathiri haki ya kupata habari.

Jana, mamlaka hizo za serikali kwa nyakati tofauti, zilitoa taarifa kwa umma zikivitahadharisha vyombo vya habari vinavyotumia watangazaji wake ambao hawana sifa za kutangaza kwa sababu hawana shahada au stashahada.

Kwa upande wa Tanzania Bara, TCRA imesema itachukua hatua ya kuwatoza faini au kufuta leseni za vyombo vya habari vinavyoajiri wasio na sifa huku Idara ya Habari (Zanzibar) ikipiga marufuku watu hao kufanya kazi ya uandishi wa habari, utangazaji na uhariri.

Hatua hiyo imetokana na vitendo vya ukiukaji wa maadili na miiko ya utangazaji, hasa kwa vyombo vya habari vya redio na televisheni, ambavyo kwa sasa vinawatumia watangazaji ambao hawana taaluma ya uandishi wa habari kuchagiza vipindi vyao.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, kuwa na watangazaji ambao hawana elimu ya masuala ya habari na utangazaji kunasababisha makosa mengi ya kutozingatiwa kwa maadili na miiko ya uandishi na utangazaji wa habari, kinyume na matakwa ya Kifungu cha 7(2)(iii) cha Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

Kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi wa Idara ya Habari wa Zanzibar, Dk Juma Mohamed alisema sera ya habari ya Zanzibar ipo wazi na imeweka kwamba ili uweze kuwa mwandishi mtu hutakiwa kuwa na kiwango cha elimu ya stashahada.

“Akizungumzia suala hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT), Kajubi Mukajanga alisema kazi ya uandishi wa habari inahitaji stadi fulani za uchakataji na ukusanyaji wa habari lakini changamoto imekuwa vya baadhi ya vyombo kuwapa watu maarufu kazi za uandishi, licha ya kuwa hawana sifa.

Alisema yapo baadhi ya mambo ambayo hayahitaji kuwa na taaluma ya uandishi kama vile kuchambua mpira, mila au masuala ya kijamii bali kuwa na uelewa wa masuala hayo huku wakisimamiwa na watu wenye weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.

“Si kosa kwa watu kuingia studio na kueleza wanachokijua, kama mtu ni mchambuzi lazima kuwe na mwandishi wa habari wa kumwongoza, tusiwafunge watu kwenda studio kueleza ujuzi wao, tutawanyima watu haki ya kupata habari,” alisema Mukajanga.