Kichere: TRA imeshindwa kufikia lengo la ukusanyaji kodi kwa miaka minne

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikipitia mabadiliko makubwa ndani ya miaka mitano, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema imeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato kwa kipindi hicho.

Tangu Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 ameshafanya mabadiliko ya makamishna wanne katika mamlaka hiyo ilia kuboresha ukusanyaji wa mapato.

Alianza kwa kumwondoa aliyekuwa Kamishna Rished Bade na kumteua Dk Philip Mpango ambaye kwa sasa ni waziri wa Fedha na Mipango.

Alipomwondoa Mpango alimteua Alfayo Kidata ambaye pia alimwondoa na kumteua Charles Kichere ambaye kwa sasa ndiye CAG na nafasi yake imechukuliwa na Dk Edwin Mhede.

Licha ya mabadiliko hayo na ya maofisa wengine wa ngazi tofauti, ripoti ya CAG ya hesabu zinazoishia Juni 30, 2019 imesema mwaka 2015/16 pekee ndiyo TRA ilipita makadirio kwa asilimia 0.13.

“Kwa ujumla, mwelekeo wa makusanyo ya mapato kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ulikuwa chini ya makadirio yaliyoidhinishwa, isipokuwa mwaka wa fedha 2015/16 ambapo makusanyo halisi yalikuwa juu ya makadirio kwa asilimia 0.13,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo, alipoulizwa juu ya suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, Richard Kayombo alisema hawezi kuongelea suala hilo kwa sasa kutokana na ripoti kuwa imewasilishwa bungeni.

Ripoti hiyo imesema kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 Mamlaka ya Mapato ilikusanya zaidi ya Sh15.74 trilioni dhidi ya malengo yaliyowekwa ya zaidi ya Sh18.29 trilioni.

“Hii inaonyesha makusanyo yalikuwa pungufu kwa Sh2.55 trilioni sawa na asilimia 14 ya malengo,” imesema ripoti hiyo.

Imesema jumla ya makusanyo hayo haihusishi Sh20.05 bilioni za vocha za misamaha ya kodi na fedha za marejesho ya kodi kutoka Hazina.

Kuhusu ufanisi katika ukusanyaji kodi kwa mwaka huo wa fedha, ripoti hiyo inasema haukuwa mzuri, kwani uwiano wa makusanyo ya kodi dhidi ya pato la ndani la taifa ulipungua mpaka kufikia asilimia 11.4 ikilinganishwa na asilimia 12.8 kwa mwaka 2017/18.

“Nashauri Serikali iongeze jitihada katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi wa makusanyo ya kodi,” alisema CAG.

Ripoti hiyo imechanganua ukusanyaji wa kodi kwa kuangalia idara tatu zikiongozwa na idara ya Forodha na Ushuru wa bidhaa iliyoongoza kwa kukusanya asilimia 40.2 ya mapato yote; ikifuatiwa na Idara ya Walipakodi wakubwa iliyokusanya asilimia 39.8 na Idara ya Kodi za Ndani iliyokusanya asilimia 20.

“Kwa ujumla, idara zote tatu za mapato zilishindwa kufikia malengo kwa mwaka huu wa fedha 2018/19,” imeeleza ripoti.

Ripoti hiyo imetaja sababu za kutoongezeka kwa mapato kuwa pamoja na kuwapo kwa kesi za kodi za muda mrefu katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB), Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) na Mahakama ya Rufaa (CAT).

“Nilibaini kesi za kodi zenye jumla ya Sh 366.03 trilioni zilizokwama kwa muda mrefu katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB), Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) na Mahakama ya Rufaa (CAT).

Alisema miongoni mwa sababu zilizosababisha kuchelewa kumalizwa kwa kesi hizi ni pamoja na ufinyu wa bajeti unaoathiri utendaji na uendeshaji wa taasisi hizo.

Alitaja pia madeni ya kodi akisema amebaini ufuatiliaji usioridhisha wa madeni ya kodi, hivyo kusababisha kurundikana kwa madeni ya kodi kwa muda mrefu.

“Nimetathmini ufanisi na jitihada za Mamlaka katika kutatua mapingamizi ya kodi na kubaini uchelewaji katika kuyashughulikia na kuyatatua.

“Uchelewaji huu una madhara katika ukusanyaji wa mapato, kwani kodi za Serikali zinashikiliwa katika mapingamizi hayo kwa muda mrefu,” imesema ripoti hiyo.

Pia CAG ametaja upungufu wa rasilimali na wakaguzi wa kodi wenye weledi akisema kumesababisha kuahirishwa kwa baadhi ya kaguzi za kikodi kulikosababishwa na ugumu wa miamala katika taarifa za walipakodi husika, hasa katika makampuni ya kimataifa na ya mafuta.

Sababu nyingine ni udhibiti usioridhisha katika kushughulikia mizigo iliyoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi nyingine.