Kichwa cha lori la mafuta ya petroli chateketea kwa moto Ruvuma

Muktasari:

Polisi mkoani Ruvuma nchini Tanzania limesema linamtafuta dereva aliyekuwa akiendesha lori la mafuta lililopata ajali kisha kichwa  chake kutekelea kwa moto ili kujua kama amefariki au la.

Songea. Lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta ya petroli limeacha njia na kugonga mti katika Kijiji cha Hangangadinda mkoani Ruvuma nchini Tanzania kisha kichwa cha gari hiyo kuwaka moto na kuteketea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 12,2019 amesema wanamtafuta dereva wa lori hilo, Hubert Mtete mwenye umri kati ya miaka 37-40 mkazi wa Njombe ili wajue kama amefariki au la.

Amesema ajali hiyo ilitolea jana Jumapili saa 4 usiku kijiji cha Hangangadinda ambapo gari aina ya Scania yenye namba za usajili T243 DTV ikiwa na shehena ya mafuta ya petrol lita 33 ,000 mali ya James Mwinuka ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Njombe Filling station ikitokea Njombe kwenda Songea ilipata ajali huku tenki likisalia pasina kuungua.

Kamanda Marwa amesema hata hivyo mafuta yapo salama bali ni kichwa kimewaka moto na mafuta yapo salama na tayari wananchi wametawanyika kumtafuta dereva huyo ambaye kwenye gari alikua peke yake ili kujiridhisha kama kuna madhara dhidi ya dereva huyo.

Aidha ameongeza kuwa tayari polisi wameimarisha ulinzi tangu jana usiku na mafuta yameanza kuondolewa na mwenye mali.