Kielelezo cha CD kesi ya Zitto chazua jambo mahakamani

Muktasari:

  •  Shahidi wa 14 katika kesi ya uchochezi inayomkabili,  Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa CD ya video iliyorekodiwa katika mkutano wa mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na waandishi wa habari  ni halisi, si ya kutengeneza.

Dar es Salaam. Shahidi wa 14 katika kesi ya uchochezi inayomkabili,  Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa CD ya video iliyorekodiwa katika mkutano wa mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na waandishi wa habari  ni halisi, si ya kutengeneza.

Wakati shahidi huyo akiwasilisha kielelezo hicho, upande wa utetezi umeitaka mahakama kutoipokea na kumfanya hakimu kuahirisha kesi hadi kesho atakapotoa uamuzi kama mahakama hiyo itapokea kielelezo hicho ama la.

Hayo yametokea leo Jumanne Desemba 3, 2019 mahakamani hapo wakati shahidi huyo, Sajenti James ambaye ni askari polisi alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Zitto.

James ni mchunguzi wa picha kutoka kitengo cha uchunguzi wa picha makao makuu ya Jeshi la Polisi.

Zitto akabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT –Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Tumaini Kwema akisaidiwa na Lilian Itemba na wakili mwandamizi, Nassoro Katuga,  shahidi huyo amedai akiwa katika majukumu yake ya uchunguzi alipokea barua iliyoambatanishwa na CD kutoka ofisi ya mkuu wa upelelezi mkoa wa Kipolisi  Kinondoni, kuombwa kuichunguza.

“Barua ile yenye kumbukumbu namba OB/IR/8291/2018 iliyotolewa Oktoba 29,  2018 iliwasilishwa kitengo cha uchunguzi na Koplo Faraja.”

“Baada ya kuipokea mkuu wangu wa kazi, SP Tumaini aliniambia niifanye kazi ya uchunguzi ili kujua kama picha zilizopo ni halali au za kutengeneza,” amesema James aliyeajiriwa polisi mwaka 1990.

Akitoa ushahidi mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi amedai baada ya kumaliza kufanya uchunguzi alibaini picha hizo zilikuwa halisi, si za kutengeneza.

“Baada ya kumaliza uchunguzi wangu niliandika ripoti na kuikabidhi sehemu husika, naiomba mahakama ipokee barua na CD kama sehemu ya ushahidi katika kesi hii,” amesema James.

Hata hivyo, upande wa utetezi wamepinga kupokewa kwa kielelezo cha CD kwa madai kuwa shahidi anayetaka kutoa kielelezo hicho hajaeleza ni namna gani video hiyo ilirekodiwa.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai nyaraka inayotakiwa kutolewa na James ni ya kielektroniki,  inatakiwa kufuata maelekezo ya sheria inayohusu utoaji wa kielelezo cha kielektroniki.

Kutokana na pingamizi hilo, hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi kesho atakapotoa uamuzi  wa kupokea kielelezo cha CD au laa.