Kigogo Chadema wilaya ya Tarime, wenzake 50 watimkia CCM

Muktasari:

Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Wilaya ya Tarime mkoani Mara nchini Tanzania, Mwita Joseph ‘white’ na wanachama wa chama hicho zaidi ya 50 wamejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa na naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara.

Tarime. Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Wilaya ya Tarime mkoani Mara nchini Tanzania, Mwita Joseph ‘white’ na wanachama wa chama hicho zaidi ya 50 wamejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Joseph na wenzake wamejiunga na CCM leo Jumamosi Aprili 4, 2020 katika ofisi za chama hicho Tarime na kupokelewa na naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara.

Wilaya ya Tarime ina majimbo mawili yanayoongozwa na Chadema ambayo ni Tarime Mjini linaloongozwa na Esther Matiko na Tarime Vijijini linaloshikiliwa na John Heche.

Waitara ambaye pia ni mbunge wa Ukonga (CCM) jijini Dar es Salaam, amekwisha kutangaza kwamba atagombea ubunge Tarime Vijijini kuchuana na Heche kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 2020.

Akizungumza baada ya kuwapokea wanachama hao wapya amesema kazi bado inaendelea kuhakikisha Chadema inafutika Tarime.

"Huu ni mwanzo wa kazi, tunawaomba waje nyumbani,” amesema Waitara aliyewahi kuwa CCM, alitimkia Chadema alikoshika nafasi mbalimbali kabla ya 2015 kuwa mbunge wa Ukonga kupitia Chadema kabla ya kurudi CCM mwaka 2018 na kugombea jimbo hilohilo la Ukonga na kuibuka mshindi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi kadi ya CCM, Joseph amesema tangu wakati wa uchaguzi wa nafasi aliyoshinda ya mwenyekiti wa wilaya hakupewa ushirikiano na uongozi uliokuwapo.

"Mpaka sasa sikuwahi kukabidhiwa vitendea kazi vya ofisi hadi kuamua kuhama wilayani Tarime kukimbilia Tabora, kutokana na kuwekewa mazingira hatarishi na waliokuwa wapinzani wangu," amesema Joseph.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Ngicho amemshukuru Joseph na wenzake kwa uamuzi huo wa kujiunga na chama tawala.

"Unapoona meli inazama ili kuokoa maisha yako unawahi kuvaa nguo za uokozi usizame baharini," amesema Ngicho.