Advertisement

Kikogwe wa miaka 90 aapishwa wakala wa uchaguzi

Wednesday October 21 2020
kikongeeepic

Mzee Daniel Wambura

Musoma. Kikongwe mwenye umri wa miaka 90, Daniel Wambura ni miongoni mawakala zaidi ya 600 wa vyama sita vya siasa katika jimbo la Tarime Mjini waliopishwa leo Jumatano Oktoba 21 kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Mbali na kikongwe  huyo, Ntori Mageta (62) pia ni miongoni mwa watu wenye umri mkubwa ambao wameteuliwa na vyama vyao kuwa mawakala katika vituo vya kupigia kura siku hiyo ya uchaguzi.

Wambura na Mageta ambao ni mawakala wa Chadema wamesema umri kwao sio kikwazo kushiriki katika shughuli hiyo muhimu.

Wambura amesema lengo lao kuu ni kutaka kuhakiksiha kuwa chama chao kinashinda katika uchaguzi huo na kushika dola huku wakitoa wito kwa Watanzania kukipigia chama chao kura nyingi.

Wambura anasema kuwa licha ya kuwa na umri mkubwa lakini anao uwezo wa kuhimili mikikimiki ya uchaguzi.

Amesema  ana uhakika wa kulinda kura za chama chake katika chumba cha uchaguzi hata kwa zaidi ya saa 24.

Advertisement

Amesema licha ya kuwa mtumishi wa umma mstaafu lakini hafurahishwi na mambo yanavyoendelea nchini na kwamba upo uhitaji wa kufanya mabadiliko ili kuleta usawa na maendeleo katika jamii.

Shughuli hiyo ya uapisho ilifanyika baada ya mawakala hao kugawanywa katika makundi mawili kutokana na wingi wao.

Kundi la kwanza kuapishwa lilikuwa la mawakala wa vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi walioapishwa katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime.

Kundi la pili lilijumuisha mawakala wa CCM, CUF na SAU ambao waliapishwa katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Tarime.

 Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo, Elias Ntiruhungwa amewataka mawakala hao kuzimgatia kiapo chao.

Ntiruhungwa amesema hakuna wakala yeyote ambaye jina lake liliwasilishwa ofisini kwake bila kuapishwa.

Amesema katika shughuli ya uapisho walialika vyama vyote vyenye mawakala.

 

Advertisement