Kikongwe aliyeoa wake 19 aoa wengine wanne

Muktasari:

Ni Raia wa Uganda, Nulu Ssemakula mwenye umri wa miaka 94 na watoto zaidi ya 100.


Kampala, Uganda. Mzee wa miaka 94 nchini Uganda ambaye ameoa wake 19 ameongeza wengine wanne na kufanya idadi ya wenza hao kufikia 23.

Nulu Ssemakula ambaye ni raia wa Uganda anayeishi katika Wilaya ya Ntungamo Magharibi mwa nchi hiyo anawatoto 100 ambao anasema kuwa vitu muhimu katika familia yake ni familia na dini.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Daily Monitor la Uganda, mke wa mwisho wa kikongwe huyo ana umri wa miaka e 24 na sasa ni mjamzito.

Gazeti hilo limeandika kuwa Ssemakula hivi karibuni mwanaume huyo aliongeza familia yake ambayo inaishi katika kaya moja kwa kuoa wanawake wanne kwa mkupuo.

Inadaiwa kuwa mwanaume huyo anayeishi katika kijiji cha Ruyonza ambacho sasa kinafahamika zaidi kama ‘kijiji cha mitala’ ni Mwislamu wa kwanza kutoka katika neoe hilo kufanya safari ya kwenda Makka mwaka 1977.

Akizungumza na gazeti hilo, Ssemakula alisema amajivunia kuwa na wanawake hao ambao wamemzalia watoto wazuri ambao mpaka sasa anaendelea kuwa hesabu lakini wamezidi 100.

“Mtoto wangu wa mwisho mwisho ana umri wa miezi i 10 sasa na mke wangu wa mwisho mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mjamzito.

“Kwa sasa naishi na watoto wangu 66 na wengine wameshaanza maisha yao. Watoto wangu wengine  wana wajukuu lakini hili halinisumbui kwani bado anatarajia kupata watoto zaidi na hata kuoa wanawake zaidi,” alisisitiza.

Gazeti hilo liliandika kwamba, wakati wa enzi ya ukoloni, babu yake mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Kashwijuma alikuwa miongoni mwa Waganda wa kwanza kutoka katikati mwa Uganda kuhamia Ankole Kusini Magharibi kwa mwaliko wa mfalme wa Ankole, Omuruki. Inaelezwa kuwa babu yake alikua mkuu wa parokia.

Baba yake Juma Tamuzadde alichagua kukaa katika Parokia ya Kyaruhuga sasa kaunti ndogo ya Bwongyera wilayani Kajara, Wilaya ya Ntungamo, baada ya watu wengi wa familia yake kuamua kurudi Buganda. Kashwijuma alikuwa ameuawa na simba.

Ssemakula alioa mke wake wa kwanza mwaka 1952, ambaye bado wanaishi pamoja mpaka sasa.

"Kwa bahati mbaya nilipoteza wanawake wangu wanne na wengine ambao wanahitaji zaidi ya uwezo wangu, niliwaacha waende. Lakini waliniacha na watoto. Bado nitaoa zaidi ikiwa bado nina miaka zaidi na hata nina watoto zaidi. Katika watoto na wake ndipo ninapopata raha yangu. Huo ni utajiri wangu wa kweli,”alisema mwanaume huyo.

Ssemakula ameanzisha msikiti na shule msingi inayojulikana kwa jina la Kiyombero ili watoto wake na wajukuu zake wasome.

Mzee huyo anajishughulisha na kilimo kwa kushirikiana na wake zake ambako chakula kinachopatikana hutumika kwa familia nzima.

"Tukiamka ni kufanya kazi tu, lazima tuhakikishe tunakamilisha kabla ya kwenda nyumbani, ndio tunafanya kila siku ya kufanya kazi. Sio kawaida kuwa sote tuko hapa, ninaishi katika mji na watoto huwa shuleni kila wakati, wakati tunapopata nafasi, tunatumia,” alisema.

 

Alisema kwa upande wa watoto wadogo wao hubaki nyumbani na ucheza pamoja wakati wengine wakienda shule na baada ya masomo ujiunga na familia nzima shambani.

“Kuna watoto kwenye migongo ya mama zao, pia wakati wengine ambao hawawezi kutembea peke yao hutunzwa na ndugu zao wakubwa. Hao ndio wale nyumbani. Wengine kadhaa wameolewa na wana familia zao au wanafanya kazi mbali na nyumba.”

Kwa upande wake Shadiah Tumuheirwe ambaye ndiyo mtoto mkubwa wa mzee huyo, alisema yeye ndiyo kiongozi wa wenzake ambaye anatoa maagizo ya kila kitu kinachotakiwa kufanyika katika boma hilo.

"Lazima nitunze kila mtu hapa. Na kila mtu ambaye ana malalamiko lazima apitishe kupitia mimi, hiyo ndio itifaki inavyodai. Ikiwa kuna mtu atakuja kwake (Ssemakula) bila kwanza kuniambia hilo haliwezi kukubalika. Wakati wa kazi ni lazima sisi sote tuamke na kufanya kazi, hakuna ubaguzi isipokuwa mke mkubwa wa mzee ambaye sisi sote tunamwita mama. Tunapika, kula, kufanya kazi pamoja na kulala chini ya paa moja.”