Kikwete afafanua alichomaanisha kwenye hotuba yake

Muktasari:

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amefafanua hotuba yake aliyoitoa Oktoba 8, 2019 katika kongamano la miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere, akieleza kuwa haikumlenga kiongozi yeyote mstaafu wala aliyeko madarakani.


Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amefafanua hotuba yake aliyoitoa Oktoba 8, 2019 katika kongamano la miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere, akieleza kuwa haikumlenga kiongozi yeyote mstaafu wala aliyeko madarakani.

Mada katika kongamano hilo lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ilikuwa, “urithi wa mwalimu Nyerere katika uongozi, Maadili, umoja na amani katika ujenzi wa Taifa” na rais huyo mstaafu alikuwa mgeni rasmi.

Katika hotuba yake, Kikwete alitaja sifa alizokuwa nazo Nyerere akisisitiza kuwa kiongozi ni sawa na mtu mwingine na haikufanyi uwe na haki zaidi kuliko wengine.

Kikwete alisema pia miongoni mwa urithi wa Nyerere ni kutotishwa na hoja na mara kadhaa akisema “hoja haipigwi rungu”.

Lakini ufafanuzi uliotolewa katika barua iliyotolewa na katibu wake e jana Alhamisi Oktoba 10, 2019, ameeleza masikitiko kuhusu upotoshaji uliofanywa na baadhi ya watu kuhusu hotuba ya rais huyo mstaafu wa Awamu ya Nne.

Inaeleza kuwa katika hotuba yake Kikwete alieleza namna anavyomfahamu mwalimu Nyerere.

“Kinachotushangaza na kutusikitisha sisi na rais mstaafu (Kikwete) ni kujitokeza kwa watu wanaopotosha ukweli kuhusu maneno yaliyosemwa na kiongozi huyu. Wapo wanaojaribu kuweka maneno kinywani mwake ambayo hakuyasema hasa waliodai alikuwa akiwasema baadhi ya  viongozi waliopo sasa,” ilieleza  barua hiyo.

Barua hiyo imesisitiza katika kongamano hilo, Kikwete alizungumzia namna anavyomfahamu Nyerere katika mambo makuu manne ambayo ni  uongozi, maadili, umoja na amani.

“Kamwe hakumzungumzia  mtu mwingine  zaidi ya  mwalimu Nyerere .Hakufanya ulinganifu  kati ya Nyerere na marais waliomfuata, waliostaafu na waliopo sasa. Hotuba yake haikutaja jina la mtu yeyote. Tunaposikia Kikwete alikuwa anamsema mtu ni jambo lililotusikitisha na kutusononesha ni uzandiki fitina na uchonganishi,” imeeleza.

 

Kwa mujibu wa barua hiyo, rais mstaafu alitazamia watu wamkosoe  kwa yale aliyoyasema kuhusu mwalimu Nyerere na sio kuingizwa  kwa masuala ambayo hakuyasema, huku akiwataka wenye maoni  wawe na ujasiri wa kuyasema sio kujificha kwenye kivuli cha hotuba yake.