MAKALA YA MALOTO: Kikwete ameongea yaliyo moyoni kwa jina la Mwalimu

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alitoa hotuba iliyozua mjadala katika kongamano la kuenzi maisha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambaye juzi alitimiza miaka 20 tangu kifo chake.

Hotuba ya Kikwete, unaweza kuiwekea kichwa cha habari “Maisha ya Mwalimu na ninavyotamani viongozi wawe.” Kikwete alimchambua Mwalimu kama kiongozi mnyenyekevu na ambaye hakuwa na kiburi na alitaka viongozi wa sasa waige mfano huo.

Japo Kikwete alilalamika kwamba kuna watu walipotosha hotuba yake, lakini kuna maneno alitamka na hatuwezi kubishana kuhusu iwapo aliyasema au hakuyasema.

Mfano, alisema: “Kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi, kujimwambafai hakukufanyi uwe kiongozi zaidi. Unapokuwa na binadamu wenzako ni wanadamu kama wewe.” Nukuu hiyo haina shaka, aliizungumza.

Kauli nyingine ambayo Kikwete aliitamka na haibishaniwi, ni ile aliyosema: “Mawazo hayapigwi rungu, mawazo yanashindwa na mawazo yaliyo bora zaidi.”

Tuongeze na hili, “Dhamana ya uongozi haikufanyi uwe mtu zaidi ya raia mwingine yeyote, haikufanyi wewe uwe na haki kuliko mtu ambaye si kiongozi.”

Kikwete pia alizungumzia ubaguzi wa kikabila na kidini. Alionya kuwa ubaguzi ukipewa nafasi, nchi haitabaki salama. Pamoja na kila eneo ambalo aliligusa na kulitolea mfano kupitia mtindo wa maisha ya Nyerere, ukweli ni kuwa Kikwete alisisitiza mno eneo la unyenyekevu, Viongozi wasijikweze, wajione ni watu wa kawaida.

Siku mbili baada ya kongamano, Kikwete alipopata nafasi ya kumzungumzia aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Apson Mwang’onda, aliyefariki dunia hivi karibuni, alisema “cheo hakikumfanya marehemu awe na kiburi.”

Ukifika hapo, huhitaji shahada ya saikolojia ili utambue kuwa Kikwete hapendi viongozi wanaojikweza, wenye kiburi. Kwa nyongeza ni kuwa mtu hanukuu maneno yasiyo na maana yoyote kwake.

Kikwete anaguswa na uongozi wenye vishindo na tambo, anataka kuona duniani kote viongozi wanakuwa ni watu wenye kukaa na raia wa kawaida kwa upendo, pasipo kuonesha matabaka.

Hapendi viongozi waweke kizuizini wakosoaji na wanaotoa mawazo tofauti. Ndiyo maana alisema mawazo hayapigwi rungu, ila mtu akitoa wazo la hovyo au dhaifu, litolewe bora na imara kulipiku lililotolewa awali.

Ukirejea miaka miwili iliyopita, Kikwete akiwa Afrika Kusini kwenye mkutano wa Jukwaa la Uongozi Afrika, alisema viongozi madarakani hawapaswi kuwaona wapinzani wao wa kisiasa kuwa maadui, bali ni washirika wa utawala bora.

Alifafanua kuwa vyama vya upinzani vipo kwa ajili ya kuvifanya vile vilivyopo madarakani visilale, kwamba kunapotokea kujisahau, angalau wapinzani watasema, hivyo viongozi serikalini wanazinduka na kurekebisha.

Hoja kuwa mawazo hayapigwi rungu, Kikwete aliwahi kuisema kwa namna tofauti huko nyuma. Alisema kuwa alipokuwa madarakani, wajumbe wa Halmashauri Kuu CCM (NEC), waliwahi kumlalamikia jinsi alivyokuwa anakaa kimya, wakati wapinzani wakiibeza Serikali kuwa haijafanya kitu chochote.

Kikwete aliwaambia wana CCM ni kazi yao kujibu pale wapinzani wanapopotosha. Alisema, kama wapinzani watasema Serikali haijafanya kitu, ni jukumu la wana CCM kuonyesha barabara, madaraja na vyote vilivyofanywa.

Akaonya kuwa wana CCM wakitegemea polisi kupambana na wapinzani, watakwisha.

Ni hoja ileile kuwa mawazo hayapigwi rungu, bali hoja inajibiwa kwa hoja. Huo ndio msimamo wa Kikwete. Na ndicho ambacho alikisema Afrika Kusini mwaka 2017.

Utaona kuwa Kikwete kila anapopata nafasi ya kuzungumzia uongozi, anagusia viongozi wasiwe wababe mbele wananchi na kwa wapinzani wao wa kisiasa, wawaache watu watoe maoni.

Hata hivyo, ukitafsiri kwa sauti ya moyoni, unaona kuwa Kikwete alimtumia Mwalimu Nyerere kufikisha maudhui ambayo amekuwa nayo moyoni siku zote.