Kilichojiri kesi ya mauaji ya mwanaharakati Wayne Lotter

Muktasari:

Jalada la kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na ujangili, Wayne Lotter (52), linalowakabili washtakiwa 16 wakiwemo raia wa Burundi,  linapitiwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kuandaliwa taarifa ya kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Dar es Salaam.  Jalada la kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na ujangili, Wayne Lotter (52), linalowakabili watu 16 wakiwemo raia wa Burundi, linapitiwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kuandaliwa taarifa ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Ijumaa Septemba 13, 2019.

Simon ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na Ofisi ya DPP inalipitia jalada la kesi hii na baada ya hapo, itaandaa taarifa kwa ajili kuihamishia kesi hii Mahakama Kuu, hivyo tu naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa " amedai wakili Simon.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.

Washtakiwa hao, wamerudishwa rumande kutokana kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 19/2017 ni raia wawili wa  Burundi, ambao ni Nduimana Jonas (40) maarufu Mchungaji na Bonimana Nyandwi.

Wengine ni Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A, Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa benki ya NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Mbali na hao, yupo Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B; Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B;  Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Washtakiwa hao, wanaokabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kumuua Lotter.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PALMS Foundation, Wayne Lotter (52).

Katika shtaka la pili, Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni, washtakiwa inadaiwa walimuua  Lotter.