Kilichosemwa bungeni kuhusu Zitto na mkopo wa Benki ya Dunia

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe

Muktasari:

Jana Jumatano Aprili Mosi, 2020 Benki ya Dunia (WB) ilifikia muafaka na Serikali ya Tanzania kutoa mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari nchini.

Dodoma. Jana Jumatano Aprili Mosi, 2020 Benki ya Dunia (WB)ilifikia muafaka na Serikali ya Tanzania kutoa mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari nchini.

Benki ya Dunia ilichelewa kutoa fedha hizo kufuatia maombi ya baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wa upinzani, akiwemo mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe waliokuwa wanataka watoto wa kike  waliopata ujauzito wakiwa shuleni waruhusiwe kuendelea na masomo kwenye mfumo wa elimu ya kawaida.

Jambo hilo lilitua bungeni jana katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka wa fedha 2020/2021 ambako Mbunge wa Mlalo (CCM) Rashid Shangazi alimpongeza Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palagamba Kabudi kwa kuwezesha mkopo huo kupatikana.

“Kwa kweli ni kazi kubwa sana imefanywa na waziri wetu. Watanzania wanashukuru sana kwa kupata mkopo huu ambao ulikuwa na figisu figisu kwa baadhi ya watu kukosa uzalendo, asante sana kwa msaada huu kwa sababu utaenda kuongeza tija katika utoaji wa elimu nchini,” amesema Shangazi.

Baada ya Shangazi kumaliza kuchangia, Spika wa Bunge, Job Ndugai alipongeza kauli ya mbunge huyo na kwamba wanamsubiri Zitto bungeni awaeleze kuwa mkopo umepatikana.

 “Tunamsubiri  mwenzetu aje atuambie mkopo tumeupata. Sasa jimboni kwake kusijengwe shule? Ndio ulivyotaka aje atujibu hapa huko Kigoma zisiende,” amesema Ndugai.

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM),  Joseph Musukuma amesema, “watu walitumia mamilioni kwenda kuharibu tusipate fedha halafu leo zimekuja. Hizi fedha mkimpelekea mgawo nitawashangaa mawaziri. Mtuangalie sisi tuliokaa kimya na kuendelea kuomba tuzipate.  Hao waliokwenda kuponda achacheni nao wasipate.”

Mkopo huo wa Benki ya Dunia utakaoanza kutolewa mwaka 2021, unatazamiwa kunufaisha wanafunzi milioni 6.5 wanaopata elimu ya sekondari huku nusu yao wakiwa wasichana.

Hao ni sehemu ya mpango wa mradi wa miaka mitano wa kuboresha elimu ya sekondari nchini Tanzania (SEQUIP).

Mwaka 2019,  Zitto na baadhi ya wanaharakati nchini Tanzania waliendesha kampeni ya kuiomba Benki ya Dunia kutotoa mkopo huo kwa Tanzania kwa madai ya kuwepo matatizo katika masuala ya haki za binadamu.

Sababu nyingine ya kuzuiwa kwa muda kwa fedha hizo ni madai ya mfumo wa elimu ya Tanzania kutoruhusu wanafunzi wa kike kuendelea na masomo pale wanapopata ujauzito.

Akizungumzia uamuzi wa Benki ya Dunia wa kutoa fedha hizo, Kabwe amesema mkopo huo umetolewa na sharti la wasichana kuruhusiwa kurudi shuleni pale wanapopata ujauzito.

“Nilipoandika barua Benki ya Dunia niliwaomba wasitoe fedha hizo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kuhofia fedha hizo zinaweza kutumika kwenye masuala ya uchaguzi badala ya kusudio lake. Sasa fedha hizo zitaanza kutolewa 2021 na asilimia 4 tu ndiyo itakayotolewa.”

“Asilimia 96 ya fedha hizo zitatolewa baada ya wakala huru kufanya ukaguzi na Benki ya Dunia kuridhia,” ameongeza Zitto.