VIDEO: Kilimo cha maparachichi chamtajirisha aliyekuwa na ajira ya kufanya usafi

Mkazi wa Njombe, Steven Mlimbila maarufu kwa jina la ‘Nemes’ alipofukuzwa kazi hakudhani kama angeweza kusimama tena.

Mlimbila aliamini ndoto zake kiuchumi zimekufa kwa sababu ya kuondolewa kazini alikokuwa ameajiriwa kama mfanya usafi.

Elimu yake ya darasa la saba ilimpa msongo wa mawazo zaidi akijua hakuna mahali kwingine atakapoweza kuomba kazi na kupata ikiwa atapeleka wasifu wake.

Lakini upepo umegeuka na sasa ana uhakika wa kuzalisha zaidi ya Sh500 milioni kwa mwaka kutokana na kilimo cha zao la parachichi.

Nemes ameajiri zaidi ya vijana 40 wakimsaidia kazi za shamba na kuendesha magari yake ya biashara hususan ya kusambaza miche ya parachichi kwa wakulima.

Anasema hajutii kufukuzwa kazi lakini zaidi anaukumbuka muda aliokaa kazini akifanya usafi kwa kulipwa ujira mdogo.

Mwaka huu 2020, amefanikiwa kuzalisha miche ya parachichi 75,000 anayouza kati ya Sh3,000 mpaka Sh5,000 kwa kila mmoja.

“Kwa kuzalisha miche tu nina uhakika wa kuvuna Sh300 milioni. Hata hivyo bado naendelea kuotesha kwa sababu mahitaji ni makubwa,” anasema.

Pia anayo miti 2,000 ya matunda hayo na katika kila mti mmoja ana uhakika wa kuvuna Sh300,000 mpaka Sh500,000 kwa mwaka.

“Hapo sasa unaweza kupiga hesabu mwenyewe kwa miti hiyo 2,000 nikiuza kwa hizo fedha nitapata shilingi ngapi? Sina tena msongo wa mawazo na familia yangu iliyo huzunika nilipofukuzwa kazi, inafuraha tena,” anasema mkulima huyo mwenye umri wa miaka 35.

Ukibahatika kumtembelea shambani kwake utabaini kuwa, amewekeza utaalamu wa kutosha jambo linalompa uhakika wa mavuno.

“Nimeajiri bwana shamba kwa ajili ya kazi hii tu, yeye amekuwa mshauri na kila siku yupo shambani anasaidiana na wafanyakazi wengine kuona hatuyumbi,” anasema Nemes.

Mafanikio yake kwenye kilimo hicho yamewahamasisha vijana wengi wa mkoa huo ambao nao wameamua kujikita katika kilimo hicho.

“Ushindani umeanza kuwa mkubwa kwa sababu vijana wengi wanakuja kujifunza na wanafungua mashamba, inawezekana kufanikiwa ukiweka bidii na kuwa mbunifu. Nimejipanga kuhakikisha sirudi nilikotoka,” anasema Nemes.

Anasema kuna wakati wanunuzi wa parachichi wamekuwa wakikosa zao hilo kutokana na uhitaji mkubwa jambo linalomuongezea nguvu ya kuwekeza.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula anasema mafanikio ya Nemes yamebadilisha mitizamo ya vijana wengi walioamua kuwekeza shambani.

“Jana (Desemba 30, 2019) alikuja yeye mwenyewe hapa nyumbani kuniletea miche ya parachichi, nami ni mkulima wa zao hili na huyu kijana amekuwa mwalimu mzuri na mfano,” anasema Mangula.

Mwaka jana Nemes alikuwa mkulima bora katika maonyesho ya Nanenane kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika mkoani Mbeya.

“Nimekuwa mkulima bora kwenye maonyesho mengi na shamba langu linatumika kama shamba darasa kwa sababu natunza mazao yangu na yamestawi kweli kweli,” anasema.

Kijana huyo ambaye alifukuzwa kazi anajivunia kuwa mwajiri, akifanya kazi na vijana wenzake zaidi ya 40.

Wakati wachache wakipata mikataba ya ujira, wengine wanafanya kazi kama vibarua wakilipwa kwa siku kulingana na uzito wa kazi walizofanya.

Ukiachilia mbali majengo ya biashara na nyumba za makazi alizojenga, Nemes anamiliki magari manne, mawili ya biashara na mawili mengine kwa ajili ya kutembelea.

Kuna wakati yeye mwenyewe huwa haamini kama ndio yule aliyelia kwa kukosa kazi.

Mafanikio yake kiuchumi yamekuwa gumzo kwa vijana wengi wakiwamo madereva bodaboda ambao wamedhamiria kuingia shambani.

“Nimenunua shamba na hapa natafuta pesa niende kwa Nemes akanipe miche, nina uhakika baada ya miaka mitatu sitakuwa hapa kiuchumi kwa sababu, soko la uhakika lipo,” anasema James Kilipamwambo, mkazi wa Njombe mjini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Parachichi, Erasto Ngole ni kati ya walimu waliompa Nemes mafunzo ya kilimo hicho.

Ngole ambaye kwenye magari yake kuna maandishi ya ‘Shikamoo Parachichi’ anasema vijana wengi wenye bidii ya kazi wamefanikiwa kiuchumi kutokana na kilimo hicho.

Siku aliyofukuzwa kazi

Bila kuweka wazi kosa na kampuni aliyokuwa akifanya kazi, Nemes anasema siku moja alienda kazini na kupewa barua ya kufukuzwa kazi.

Barua hiyo ilimpa msongo wa mawazo hasa kutokana na hali ya uchumi wa familia. “Familia niliyozaliwa ilikuwa maskini sana, mie mwenyewe baada ya kuoa bado niliishi maisha ya chini. Kufukuzwa kazi kilikuwa kidonda kikubwa,” anasema Nemes.

Nemes anasema alirejea nyumbani kwa unyonge na kumwambia mkewe kuhusu taarifa hiyo ngumu.

Sababu ya kufukuzwa kazi

Nemes ambaye alikuwa analisha Sh45,000 kwa mwezi alifukuzwa kazi mwaka 2007 kwa kosa la kuchelewa.

“Sikuchelewa kwa maksudi na sikupewa nafasi ya kujieleza, siku hiyo radi ilipiga na kuua watu wawili kijijini hivyo kama mwanajamii nilipitia kwenye taharuki kabla sijafika kazini,” anasema.

Anasema siku hiyo alisamehewa lakini siku ya pili akachelewa tena na hapo bosi wake aliagiza akifika getini asifunguliwe. “Nililazimisha, nikachukua fagio kufanya usafi lakini nikafukuzwa.”

Maisha baada ya kukosa kazi

Anasema alirejea nyumbani akifikiria kazi ya kufanya na kwa wakati huo alikuwa amepewa msaada wa kuishi kwenye nyumba ya rafiki yake.

Kwa sababu familia yao ilikuwa na ardhi, aliamua kuwekeza kwenye kilimo kwa kuanza kupandikiza miti ya mbao kisha kuuza.

“Niliuza miche kidogo kidogo, mtaji halikuwa jambo gumu kwa sababu ardhi ilikuwa ya wazazi, ilikuwa ninapopata faida naongeza idadi na ninanunua shamba. Nikaanza kupanda miti yangu mwenyewe,” anasema kijana huyo.

Kilimo cha Parachichi.

Mwaka 2010 Nemes anasema alipata ushauri kutoka kwa rafiki zake kwamba wanaweza kuachana na kilimo cha miti ya mbao na badala yake waanzishe kilimo cha matunda.

“Ukipewa mawazo unayafanya tu hata kama huna uhakika, nilikubali kupanda miche ya parachichi huku nikiwekeza kwenye kuotesha miche,” anasema.

Japo hakuwa na uhakika wa faida atakayopata kwenye kilimo hicho, aliweka bidii akitumia mbolea ya samadi na mboji jambo lililosababisha miti yake kukua vizuri.

Anasema baada ya miaka minne alianza kuvuna parachichi na kadri siku zilivyo kuwa zinasogea ndivyo soko lilipozidi kuwa kubwa.

“Kwa hiyo nilipoanza kuvuna soko pia likawa kubwa nikaona fursa na hapo ndipo nilipoanza kuongeza bidii,” anasema.

Anasema alianza kuvuna matunda na kwamba kadri siku zilivyosogea ndivyo soko la zao hilo lilivyokuwa linaongezeka.

“Nilianza kuuza kwa faida na hapo sasa maisha yangu yalianza kubadilika kwa kasi. Nilifanikiwa kufungua kampuni yangu inayoitwa Nemes Green Garden,” anasema Nemes.

Anasema mpaka sasa kampuni hiyo inafanya kazi huku akiwa na uhakika wa kupata fedha nyingi kwa zao hilo.

Mafunzo Kenya

“Nilienda Kenya kujifunza kilimo cha parachichi, nilizungukia mashamba mengi yaliyolimwa kisasa na kilimo hicho nimekuwa nikilima hapa,” anasema mkulima huyo mashuhuri.

Anasema kwa sasa anamiliki mashamba katika kijiji cha Maheve na kote, analima zao hilo.