Kilio cha uchaguzi huru, vyama vyaitaka Takukuru, polisi mezani

Oktoba 2020 kutafanyika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, wawakilishi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar.

Uchaguzi utafanyika kuwapata viongozi hao watakaohudumu kwa miaka mitano kama ilivyo kwa waliopo waliochaguliwa Oktoba 25, 2015 muda wao kufikia hatamu Kikatiba.

Maandalizi ya uchaguzi huo yameshaanza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza awamu ya pili ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura pamoja na kuweka wazi daftari la wapiga kura la 2015 ili walioandikishwa waweze kuhakikiwa.

Wakati NEC ikiendelea na maandalizi ikiwamo kuwakutanisha wanasiasa hivi karibuni kujadili suala la uandikishaji wapiga kura, Baraza la vyama vya siasa nchini linatoa wito wa kufanyika kwa mikutano kama hiyo ya tume ili kuwawezesha kujiandaa na uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa baraza hilo, John Shibuda anatumia fursa ya mkutano wa NEC kuitaka Serikali kupitia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuitisha kikao cha baraza ili kujadiliana na wadau mbalimbali.

Shibuda anasema ili uchaguzi ukawe huru na haki kama alivyoahidi Rais John Magufuli lazima kama baraza wakutane na kuangalia yapi ya kufanyiwa kazi kabla na baada ya uchaguzi vinginevyo ahadi ya Rais Magufuli haitoweza kutekelezwa.

Ahadi ya uchaguzi huru na wa haki ilitolewa na Rais Magufuli Januari 21 mwaka huu wakati akizungumza na mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya.

Ahadi kama hiyo pia ilirudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi wakati alipohutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.

Shibuda anasema kuna haja ya vyombo vinavyohusika na uchaguzi kama polisi na Takukuru wakahudhuria katika kikao hicho ili kubadilishana mawazo na hivyo kuufanya uchaguzi ukawe huru na haki.

Anasema kuna umuhimu mkubwa wa vyama vya siasa kukutana na vyombo hivyo kwani licha ya sheria kuwataka kukutana mara nne kwa mwaka lakini tangu kikao cha mwisho kufanyika Juni mwaka jana hadi sasa hakuna kilichofanyika pasina sababu ya msingi kutolewa.

Juzi Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenereali John Mbungo alizungumza na wahariri na kusema kuwa taasisi yake imepokea taarifa za kuwepo kwa watu walioanza kampeni za uchaguzi.

Mkurugenzi huyo aliahidi kuwachukulia hatua kwa kuwa wanakiuka sheria na kanuni za uchaguzi.

“Ukiondoa juhudi nzuri za tume ya uchaguzi lakini polisi hawajakutana na wadau wa siasa, Takukuru haijakutana na wadau wa siasa, Tamisemi haijakutana na wadau wa kisiasa na vikao hivyo ni muhimu kwani usipoziba ufa utajenga ukuta,” anasema Shibuda ambaye ni katibu mkuu wa Ada-Tadea

Anasema, “kuvunja amani ni kazi rahisi lakini kuijenga ni ngumu” na kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia vikao hivyo ili kwenda kuufanya uchaguzi huo kuwa huru na wa haki kama alivyoahidi Rais Magufuli.

Shibuda anatumia fursa hiyo kumweleza Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, Tixson Nzunda ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo wa NEC kuwa anahudhuria mara kwa mara pamoja na kuishauri serikali ili baraza liweze kuitishwa.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muhab anayesema kutofanyika kwa kikao kunarudisha nyuma utekelezaji wa kauli ya Rais kwa kuwa, “vikao vinatufanya tunazungumza, polisi, Takukuru na wengine na lazima tutofautiane tunapozungumza ili kuboresha mahusiano yetu.”

“Kutofautiana katika kuzungumza hakuwezi kutufanya tusizungumze kwani kuna adui ambaye ni chuki inatufanya tusizungumze na bila kufanya hivyo tunakwenda kuharibu mtengamano wa umoja wetu hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu,” anasema Muhab.

Muhab anaungana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Bara, Benson Kigaila anayesema, “tunapokwenda katika uchaguzi mkuu, hoja inaweza kuwa siyo baraza hoja ni kama kuna vyombo vimeundwa ili kukutanisha vyama ni muhimu kuvikutanisha kwani haitakuwa na tija kama isipokutanisha.”

“Shida inakuja kipindi baraza lilipokuwa linaundwa lilikuwa na malengo fulani kwa watu fulani lakini ikimalizika, inashindwa kuendelea na mimi nadhani ni muhimu likikutana kwa sababu ni chombo kilichopo, likae lifanye shughuli yake,” anasema Kigaila.

Kauli ya Serikali

Katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, Tixson Nzunda anasema baraza hilo lipo kisheria na kusema tayari amekwisha kumweleza msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao cha baraza huku akisisitiza kwamba lazima kuwe na agenda ya kipi kinakweza kuzungumzwa.

Naye Jaji Mutungi anasema kikao cha baraza kinaweza kufanyika kati ya Aprili na Mei mwaka huu iwapo kamati ya uongozi ya baraza itapanga na wala hakuna tatizo lolote la baraza hilo kukutana na kujadili kulingana na agenda zitakazokuwa zimeandaliwa.

Mikoa 12 ya awali

Katika mkutano huo Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage anasema kwamba maboresho ya daftari la wapiga kura awamu ya pili yatafanyika kuanzia Aprili 17 hadi Mei 4 mwaka huu kwa mgawanyo wa awamu mbili.

Anasema awamu ya kwanza itakuwa kuanzia Aprili 17 hadi 19 ikihusisha mikoa 12 yenye vituo vya kuandikisha 2005 kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.

Awamu ya pili itaanza Mei 2 hadi Mei 4 ikiwa na vituo vya uandikishaji 2001 kwenye mikoa 14 ya Tanzania Bara na Visiwani. Mikoa hiyo ni; Katavi, Singida, Mbeya, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Rukwa.

“Jumla vituo vya kuandikisha wapiga kura vitakavyotumika katika awamu hii ni 4,006 badala ya 8,031 tulivyowaeleza (vyama vya siasa) awali. Kati ya hivyo, vituo 3,956 vitakuwa Tanzania bara na 50 Zanzibar,” anasema Jaji Kaijage.

Anasema uboreshaji huo utafanyika katika kila kata ambapo kutakuwa na mwandishi msaidizi na mwendeshaji wa mashine ya kuandikisha ya BVR Kit ambao kwa pamoja watakuwa na orodha ya vituo vyote katika kata husika.

Jaji Kaijage anasema wakati uandikishaji huo ukiendelea, watabandika orodha ya wapiga kura walioandikishwa awamu ya kwanza na mpiga kura atakayekuwa amehakiki taarifa zake na kuhitaji kufanyiwa maboresho ana mpiga kura anayehitaji kumwekea pingamizi mpiga kura mwingine, atatakiwa kwenda kituo cha kata husika kilichopangwa.

“Shughuli hii ya uwekezaji wazi wa daftari litawahusu wapiga kura wote, wakiwamo wale walioandikishwa mwaka 2015 na wale walioandikishwa katika awamu ya kwanza ya uboreshaji,” anasema Jaji Kaijage.

Jinsi ya kuhakiki taarifa

Mwenyekiti huyo anataja njia tatu zinazoweza kutumiwa na mpiga kura kuhakiki taarifa zake ni kufika kituo alichojiandikisha, kutumia simu ya mkononi atapiga namba *152*00# na kufuata maelekezo yatakayomwezesha kuhakiki taarifa zake. Huduma hii ni bure.

Anasema kwamba njia nyingine ni kupitia tovuti ya tume (www.nec.go.tz) mpiga kura atahakiki taarifa zake katika sehemu iliyoandikwa “uhakiki” na kuendelea au kupiga simu kituo cha huduma kwa mpiga kura, ni bure kwa namba 0800782100.