Kina Mbowe wakata rufaa Mahakama Kuu

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba wamekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 10, 2020.

Dar es salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba wamekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 10, 2020.

Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa tisa alikuwa Dk Vicent Mashinji aliyehamia CCM Februari 18, 2020 akitokea Chadema alikokuwa katibu mkuu kuanzia mwaka 2016 hadi Desemba 2019, wote walitakiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kifungo cha miezi mitano jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.

Uamuzi wa kuwatia hatiani ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi.

Mbali na Mbowe, wengine ni katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Halima Mdee (Kawe); John Heche (Tarime Vijijini); Ester Bulaya (Bunda).

 

Kwa nyakati tofauti walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo

Katika rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 inayoonyesha kupokelewa Mahakama Kuu Masjala ya Dar es salaam Aprili 8, 2020, inaonyesha warufani nane isipokuwa Dk Mashinji.

Baadhi ya mambo waliyopinga katika hukumu hiyo ni Mahakama ya Kisutu kufanya makosa ya kisheria kufikia maamuzi ya kesi ya msingi bila ya upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo shaka.

Wamedai Mahakama ya Kisutu ilikosea kwa kushindwa kufanya mchanganuo vizuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa.

Sababu nyingine  waliyoianisha ni mahakama kushindwa  kuainisha viini vya makosa dhidi ya mashtaka na kuwahukumu ndivyo sivyo na kutozingatia utetezi wa washtakiwa.

Hoja nyingine ni kupinga hukumu hiyo kutokana na Mahakama kushindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo au ushiriki wa baadhi ya watuhumiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye shtaka la 2,3 na 4.

SOMA ZAIDI