Kisa corona, Ma RPC na RPO watakiwa kuwapa dhamana mahabusu

Naibu waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania yawaagiza makamanda wa polisi nchini (RPC)kuhakikisha wanatoa dhamana mahabusu waliokidhi vigezo ili kuondoa msongamano katika vituo hivyo. Pia wakuu wa magereza wametakiwa kuharakisha upelekwaji wa kesi za watuhumiwa waliopo katika magereza ili kuondoa msongamano wakati huu Serikali inapambana na mlipuko wa ugonjwa corona.

Dar es Salaam. Naibu waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amewaagiza  makamanda wa polisi nchini humo (RPC), kuhakikisha wanawapa dhamana mahabusu waliokidhi vigezo ili kuondoa msongamano katika vituo hivyo.

Agizo hilo la Masauni liliwahusu pia wakuu wa magereza nchini (RPO) ambao wametakiwa  kuharakisha upelekwaji wa kesi  za  watuhumiwa waliopo katika magereza ili kuondoa msongamano wakati huu Serikali inapambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumamosi Aprili 4, 2020 na wizara hiyo imeeleza Masauni ametoa maagizo hayo  alipofanya ziara ya kushtukiza katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Dodoma na kuibaini uwapo msongamano wa mahabusu katika vituo hivyo.

Katika ziara hiyo, Masauni  alifanikiwa kuzungumza na baadhi ya mahabusu ambao kesi zao zilizoonekana zinadhaminika na wengine waliruhusiwa kufuatia ujio wa naibu waziri huyo.

“Maagizo ya Serikali na wataalamu wa afya ni kuepusha msongamano sasa nimetembelea kituo hiki cha kati nimekuta mahabusu wengine wamekaa siku 14. Kuna mahabusu mmoja nimekuta wamemuweka siku tatu hapa kosa lake wamemkamata tu anapita nje ya bunge hii siyo sawa,” amesema

“Sasa natoa maagizo kwa makamanda wa polisi nchini katika kukabiliana na ugonjwa wa corona wahakikishe mahabusu wote ambao kesi zao zinadhaminika watolewe,” amesema Masauni