Kitakavyokuwa kituo kipya cha mabasi Dar

Katibu Mkuu tamisemi (kushoto) akikagua Ujenzi wa Kituo kipya cha Mabasi ya mikoani kinachojengwa Mbezi jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umemueleza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Nyamhanga kuwa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi ya mikoani eneo la Mbezi umefikia asilimia 57, utakamilika Julai 2020.

Dar es Salaam. Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umemueleza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Nyamhanga kuwa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi ya mikoani eneo la Mbezi umefikia asilimia 57, utakamilika Julai 2020.

Wameeleza hayo leo Alhamisi Februari 27, 2020 wakati Nyamhanga  alipotembelea na kukagua ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa kwa Sh50.9 bilioni.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana mchumi wa Jiji hilo, Wambura Yamo amemueleza  Nyamhanga kuwa jengo hilo litakuwa na ofisi za Serikali  ikiwamo polisi, uhamiaji, TRA( Mamlaka ya Mapato Tanzania), pamoja na kituo cha afya.

"Fremu za maduka, eneo la kuegeshea magari binafsi takriban 200 kwa wakati mmoja  limeshakamilika. Eneo la kuegesha mabasi lipo katika hatua za mwisho kukamilika, " amesema Yamo.

Amesema stendi hiyo ya kisasa  itakuwa kituo cha kutoa huduma za pamoja , akibainisha kuwa hivi sasa mkandarasi  anayetekeleza mradi huo kampuni ya  Hainan International anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anamaliza kwa muda uliopangwa.

Nyamhanga amesema licha ya mradi huo kukumbwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wake, ameridhika na maendeleo yake huku akitamka mkandarasi kuongeza juhudi.

" Malengo ya miradi kama hii ya kimkakati inasaidia kuziongeza uwezo halmashauri kujitegemea na kuongeza mapato, mradi huu ukikamilika halmashauri ya Jiji itapata kodi Sh7 bilioni kila mwaka," amesema Nyamhanga.

Nyamhanga ametembelea pia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambao ni ujenzi wa barabara Korogwe hadi Maji Chumvi yenye urefu wa kilomita 10, kwamba ujenzi umeshakamilika wanamaliza vitu vidogo.