Kitendawili cha intelijensia mikutano ya kisiasa kigumu

Dar es Salaam. Neno ‘taarifa za kiintelijensia’ linalotumiwa na polisi kama sababu za kuzuia mikutano ya viongozi wa kisiasa kama wabunge, limeibua maswali na linaweka changamoto katika suala la usalama nchini.

Kwa nyakati tofauti, polisi wa maeneo tofauti wamekuwa wakizuia mikutano ya kisisasa, hasa ya vyama na viongozi wa upinzani, kwa maelezo ya kupata taarifa za kiintelijensia zinazoonyesha viashiria vya uvunjifu wa amani.

Hali hiyo imejitokeza tena juzi wakati polisi walipozuia mkutano wa mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kwa sababu hizo za kiintelijensia.

Katika barua kwa Mwakajoka, kamanda wa polisi wa Wilaya ya Momba, G.S Sarakikya amesema mkutano huo utaruhusiwa pindi hali ya amani itakaporejea.

Barua hiyo ya Februari 20, Sarakikya anasema: “Nakujulisha umekatazwa kufanya mkutano wa hadhara uliopanga kuufanya tarehe 23.02.2020 saa 07:00 mchana hadi saa 12:00 jioni katika viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma.

“Hii ni kutokana na uwezekano wa kutokea vitendo vya uvunjifu wa amani katika mkutano huo kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia tulizonazo. Hivyo basi unashauriwa ufanye mkutano huo baada ya hali ya usalama na amani kurejea.”

Sababu zilizotolewa katika barua hiyo zinafanana na nyingine za sehemu kadhaa ambazo jeshi hilo limekuwa likitoa kuzuia mikutano.

Wakati sababu zinafanana, hata wanaozuiwa kufanya mikutano hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa, ni wa upande mmoja; vyama vya upinzani, isipokuwa pale wabunge kutoka vyama viwili vilivyo mkoa au wilaya moja wanapoomba pamoja.

Mwenendo huo umekuwa ukiibua maswali.

Hoja nyingine ni jinsi maneno “viashiria vya uvunjifu wa amani” yanavyotumika kila mara na sehemu tofauti, hali inayoweza kutoa tafsiri hasi ndani na nje kuhusu hali ya usalama nchini.

Miongoni mwa matukio ya aina hiyo ni lile la polisi mkoani Kigoma kuzuia mkutano wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe uliokuwa ufanyike Januari 17, 2020 kwa sababau za kiusalama.

Zuio la Zitto lilitanguliwa na zuio la mkutano wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe uliokuwa ufanyike Morogoro Juni 16, 2019 kutokana na sababu zilezile za usalama.

“Kazi ya polisi ni kutupa ulinzi,” alisema Dk Hellen Kijo-Bishimba, mkurugenzi mkuu wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

“Kama wameona taarifa za kiintelijensia si nzuri, kazi yao ni kuzuia kwa kutoa ulinzi wa kutosha. Lakini tunachokiona haki za kisiasa na kiraia zinavunjwa.”

Mwanaharakati huyo mkongwe alisema amri za polisi kuzuia mikusanyiko zimejikita zaidi katika eneo la siasa.

“Tangu wamepata taarifa hizo za kiintelijensia wamewakamata wangapi na hatua gani wamezichukua? Hatujawahi kusikia wamekamatwa (wanaotishia uvunjifu wa amani),” alisema Bisimba.

“Kama nchi yetu si salama wakati kila siku tunasema ni nchi ya amani, sisi wananchi wanatupa hofu na wale wa nje wanaona hali ya usalama si nzuri kwa hiyo kunakuwa na shida.”

Naye mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alisema uhuru wa Taifa alioupigania hayati Mwalimu Julius Nyerere ulipatikana kwa njia ya mazungumzo na mikusanyiko bila kumwaga damu.

Alisema licha ya Katiba kuruhusu mikusanyiko na hata Rais John Magufuli kusema kila mbunge na diwani kufanya mikutano katika maeneo yao, bado kumekuwa na shida kwa polisi kuizuia hasa ile ya upinzani. “Hawa wanaotakiwa kutekeleza kwa kusimamia hayo-- Jeshi la Polisi ndio haohao wanaizuia. Lakini hali haiko hivyo kwa wabunge wa chama tawala (CCM), mbona katika mechi za Simba na Yanga hawazizuii kwa taarifa za kiintelijensia,” alisema Mbatia

Lakini msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime aliiambia Mwananchi jana kuwa mikusanyiko, maandamano au mikutano ya hadhara inatakiwa kufuata taratibu za kisheria.

“Wasimamizi wa sheria kama polisi wamepewa maelekezo ya kisheria na taratibu za kufuata wakati wote wa kusimamia mikusanyiko hiyo na si kufuata hisia za mtu au watu,” alisema Misime.

Kuhusu uwezekano wa taarifa hizo kuangaliwa kwa mtazamo hasi na mataifa mengine duniani, Misime alisema: “Kama jeshi huwezi kuuza ramani ya vita, masuala mengine ni kiushahidi hivyo huwezi kuanika hadharani.”

Hoja ya zuio la mikutano imekuwapo kwa muda mrefu. Novemba 21, 2000, aliyekuwa Jaji Mkuu, Barnabas Samatta alisema polisi hawaruhusiwi kuzuia mikutano au maandamano kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Samatta aliwaambia wabunge waliokusanyika Dodoma baada ya uchaguzi mkuu kwamba, msimamo wa mahakama kwa wakati huo ni kuwa si kazi ya polisi kutoa kibali kwa chama cha siasa kufanya mkutano au maandamano.

Sakata la Mwakajoka

Lakini Mwakajoka aliiambia Mwananchi jana kuwa hii ni mara ya tatu kwa polisi kumzuia kufanya mikutano jimboni kwake, akisema mara ya kwanza ilikuwa Julai 2019 na baadaye Oktoba 2019.

“Hii Intelijensia ni kichaka tu na sasa hivi (OCD) anatumika kisiasa ili sisi tushindwe kufanya mikutano na tushindwe kuwasiliana na wananchi wetu,” alisema mbunge huyo.

“Kama kuna intelijensia yoyote inayoonyesha kuna tatizo, huko baadaye yeye aje alinde mkutano na kama anashindwa kulinda mkutano atueleze ili dunia ijue hakuna usalama.”

Mwakajoka alisema tayari amemwandikia barua Kamanda wa Polisi wa Songwe akimtaka atengue amri ya OCD wake.

“Bila (kufanya) hivyo nitampeleka OCD mahakamani, si kwa cheo chake bali yeye kama yeye kwa jina lake,” alisema Mwakajoka.

Hata hivyo, kaimu kamanda wa polisi wa mkoa, George Salala alisema OCD yuko sahihi kutokana na mazingira kuonyesha hayako salama na hali ikitulia mbunge huyo ataruhusiwa kufanya mikutano yake kama kawaida.

“Mikusanyiko ya kisiasa ni haki yao na wananchi wana haki ya kuzungumza na mbunge wao, lakini vyombo vya usalama navyo vina wajibu wa kulinda. Sisi tunamwamini OCD anapokuwa anafanya kazi katika eneo lake,” alisema Salala.

Sheria ya polisi

Naye Kamanda Misime alisema lengo la sheria ni kuhakikisha haki inatendeka na usalama wa nchi unazingatiwa bila kufuata matakwa ya watu.

Alisema sheria ya polisi na polisi wasaidizi Sura 322 inaelekeza namna ya kusimamia mikutano ya kisiasa na kwamba OCD anapopokea taarifa ya mkutano kutoka chama cha siasa anaweza kuukataza usifanyike kutokana na sababu mbalimbali ikiwapo za kiusalama na kwamba endapo chama husika hakitaridhika kinapaswa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Maana ya Intelijensia

Kuhusu dhana hiyo, wakili wa kujitegemea wa mjini Moshi, Patrick Paul alisema tafsiri ya intelijensia ya polisi ni kitendo cha polisi kukusanya taarifa kutoka kwa wasiri wao kuhusu uwepo wa uvunjifu wa amani.

“Ni ile kufanya ufuatiliaji ukusanyaji wa taarifa ambazo baadaye huzichambua na kuhitimisha kitisho cha uhalifu au kuthibitisha hakuna kitisho. Kwa sehemu kubwa ni taarifa za siri,” alisema Paul.

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema alisema neno intelijensia ya polisi linatumika kimkakati ili kuua upinzani nchini kwa kuhakikisha mikutano yao haifanyiki.

“Hakuna kitu kinaitwa intelijensia ya polisi nchi hii bali huwa kuna uhuni dhidi ya demokrasia na uhuru wa mamlaka ya Katiba kuhusu watu kukutana na kupashana habari,” alisema Lema.

Mbunge huyo wa Arusha Mjini (Chadema) alitahadharisha kuwa kinachoendelea nchini kinawapeleka watu katika fikra nyingine tofauti na kusisitiza siku za kudai haki zinakuja.

“Siku ya mwisho hawatachukua haki za watu ila wanaonyang’anywa haki watadai haki na wakidai haki, wao (polisi) wakifikiri ni fujo nchi ikifika huko itaingia katika hatua mbaya zaidi,” alisema.

“Tunangojea kwanza hasira zikusanyike na ari ya watu iimarike. Nina uhakika iko siku hili litaisha na si muda mrefu. Sisi kama chama tunaona na sisi si wapumbavu.”

Shibuda, Mbatia wang’aka

Kuhusu suala hilo, mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda alisema kuzuia mikutano hakukubaliki kwa kuwa kunakinzana na kauli ya hivi karibuni ya Rais Magufuli mbele ya wanadiplomasia kwamba uchaguzi mkuu mwaka huu utakuwa huru na haki.

“Kunahitajika hali nzuri ya kufanya siasa kwa kuwa dalili ya mvua ni mawingu. Mimi wito kwa vyombo vya dola na taasisi zote, kila wilaya na mikoa waanze kutengeneza mazingira ya kuithaminisha kauli ya Rais aliyoitoa kitaifa na kimataifa kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki,” alisema Shibuda.

“Migogoro ikizidi katika jamii inakuwa fujo,” alisema.