USHAURI: Kitwanga, Mwijage wampa somo Lugola

Dodoma. Mawaziri watatu ambao walipoteza nyadhifa zao kwenye serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli wamempa somo Kangi Lugola baada ya kuvuliwa uwaziri.

Wamempa ushauri wa uzoefu wao baada ya Lugola kuvuliwa wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani, wiki iliyopita.

Pia mawaziri hao waliotumbuliwa na Rais Magufuli wametoa maoni yao kwa nini hawazungumzi bungeni au wanapoongea mara nyingi wanatetea upande wa Serikali.

Mawaziri hao wa zamani ni Charles Kitwanga (Mbunge wa Misungwi), Charles Mwijage (Mbunge wa Bukoba Vijijini) na Jumanne Maghembe (Mbunge wa Mwanga).

Rais Magufuli aliwaondoa watu hao kwa sababu mbalimbali katika nyadhifa zao baada ya kuona wameshindwa kwenda na kasi yake katika vipindi tofauti tangu aingie madarakani mwaka 2015.

Lugola aliondolewa kutokana na kashfa ya kuingia makubaliano ya kuagiza vifaa vya moto bila ya idhini ya bunge na kampuni moja ya Romania.

Nafasi ya Lugola, ambaye atarudi bungeni kama mbunge imechukuliwa na mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene.

Ushauri wa Kitwanga

Kitwanga, ambaye alikuwa waziri wa kwanza wa wizara ya mambo ya ndani katika utawala wa Rais Magufuli amemtahadharisha Lugola kwamba anahitaji kutulia kwanza bungeni.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kitwanga alisema; “Lugola atulie tu, asianze kupaparika, asianze kuuliza maswali, akae siku moja, siku mbili.”

“Maisha lazima yaendelee, ni kama amejikwaa, kujikwaa sio kuanguka kwa hiyo atulie, asiwe na shida yoyote, mbona sisi tulifukuzwa na maisha yanaendelea,” alisema Kitwanga, ambaye alivuliwa uwaziri mwaka 2016 kwa kosa la ulevi bungeni.

Kitwanga alisema jambo muhimu ni kutimiza wajibu kwa kuzingatia maslahi ya taifa,

“Sioni tatizo lolote, mbona (Rais mstaafu Ali Hassan) Mwinyi aliwahi kujiuzulu uwaziri baadaye akaja kuwa rais, haya mambo ni ya kawaida tu, kama kweli uko ‘serious’ (makini) na unajua unachokifanya huwezi kutetereka.”

“Kitu kikubwa unasamehe, watu kama sisi, unaonewa kabisa, unajua kabisa unaonewa lakini unakwenda kanisani na kumwomba mwenyezi Mungu kwani dunia inazunguka kwenye mhimili wake, haiwezi kubaki palepale, itakupitisha kwenye mema, kwenye raha, wewe vumilia na timiza wajibu wako.”

Kitwanga aliongeza kwa upande wake anatetea nchi na kuwatetea watu wa jimbo lake la Misungwi.

“Nikiona Serikali inashambuliwa na hakuna anayetetea basi mimi najitupa kusaidia. Lakini kama hakuna cha kuchangia nakaa kimya si lazima kuzungumza ukiwa bungeni,” alisema Kitwanga.

Neno la Mwijage

Aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara, Mwijage alisema suala la kuchangia bungeni inategemea hulka na staili ya mbunge husika.

Alisema kwa upande wake hajabadilika hata baada ya uwaziri wake kutenguliwa kwa sababu yeye huchangia kwa hoja na si kupiga kelele.

Alitolea mfano wa wakati wa bunge la bajeti la mwaka 2019/2020 katika mchango alishauri Serikali kuhusu kuboresha mpango wa `Blue Print’ .

“Mimi sijabadilika ni yule yule kabla ya kuteuliwa kuwa waziri. Hata ukitaka ushahidi angalia video zangu utaona uchangiaji ni ule ule wa hoja na si kupiga kelele,” alisema Mwijage, ambaye alivuliwa uwaziri mwaka 2018.

Mwijage alisema uchangiaji wa kila mbunge unategemea hulka na staili na kwamba uchangiaji wake kabla ya kuwa waziri na baada ya kutenguliwa umekuwa si wa kupingana na Serikali bali wa kuwasilisha hoja.

Alisema kwa kuwa waziri kumemfanya kujifunza jinsi ya kutoa hoja kwa Serikali na sio kupiga kelele bungeni.

Alitoa mfano wa mbunge anayepeleka hoja ya kutaka kununuliwa meli katika jimbo lake wakati wa mkutano wa bajeti wakati tayari kuna randama imeshapitishwa.

Ufafanuzi wa Maghembe

Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe alikiri kutoa michango ya kuisaidia serikali pale inapobidi kwani licha ya ubunge bado ni Mtanzania.

“Nimehudumu katika nafasi ya ubunge kwa miaka 20 sasa na kati ya hiyo 13 nikiwa katika baraza la mawaziri, lakini mimi ni mwanasayansi lazima nisimamie taaluma, ndiyo maana bado nafikiria kuwa iko haja ya kugombea ubunge tena ili niendelee kutoa mchango wangu kwa nchi yangu,” alisema Maghembe, ambaye alivuliwa uwaziri mwaka 2017.

Wachambuzi walonga

Akizungumzia vitendo vya mawaziri hao wa zamani, mratibu wa taasisi zisizo za kiserikali mkoani Dodoma (Ngonedo) Edward Mbogo alisema kinachofanya kusimama kama sehemu ya serikali ni woga.

Mbogo alisema baadhi ya wawakilishi hao bado wanaendelea kuamini kuwa ipo siku watarudishwa katika baraza la mawaziri hivyo wanafanya kwa kumfurahisha mtoa maamuzi.

Mawaziri wengine waliotumbuliwa kwenye serikali ya awamu ya tano kwa nyakati tofauti ni pamoja na Profesa Sospiter Muhongo (Nishati na Madini), Mwigulu Nchemba, Joseph Kakunda (Viwanda), Nape Nnauye na Naibu wake Anastazia Wambura (Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo) na Dk Charles Tzeba (Kilimo).

Wengine ni January Makamba (Muungano na Mazingira),Gerson Lwenge (Maji), Naibu Waziri Ramo Makani (Maliasili na Utalii) na Edwin Ngonyani alihudumu nafasi ya naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Bunge `kumisi’ uenyekiti wa Zungu

Mambo yatakayokosekana katika Bunge hili ni staili ya uongozaji wa aliyekuwa mwenyekiti Mussa Zungu.

Wabunge watazikosa staili hizo mbele ya kiti cha Bunge lakini huenda zikaja kwa aina yake kwani mbunge huyo wa Ilala amekabidhiwa nafasi ya kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.

Katika mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais Magufuli, mbunge huyo amepewa nafasi hiyo ambayo Waziri wake Simbachawene amepelekwa mambo ya ndani ya nchi akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Lugola.

Hakuna mbunge aliyelala, hakuna waziri aliyelala wala kusinzia pale Zungu alipokuwa amekalia kiti cha Spika akiongoza vikao, maneno yake ya tambo, vitisho vilivyojaa utani mwingi vilimtambulisha na kumfanya akose mtu wa kumlaumu kwa pande zote.

Mtaalamu huyo wa masuala ya anga, alikuwa akitumia kiti chake kuwafanya hata wapinzani kucheka kwani katika maeneo ambayo alihisi hayana madhara kwa Serikali, aliwapa nafasi zaidi upinzani ili mwisho wa siku awanyime nafasi kwenye mijadala yenye kuikosoa serikali.

Mawaziri watapumua

Hakuna mwenyekiti, Spika au Naibu spika ambaye alikuwa akiruhusu maswali mengi ya nyongeza kujibiwa ndani ya kipindi cha maswali na majibu kama siyo Zungu.

Naibu Mawaziri Juma Aweso (Maji) na Subira Mgalu (Nishati) ni miongoni mwa walioitwa mbele mara nyingi zaidi kujibu maswali ya wabunge hasa yale ya nyongeza lakini yeye akidai ni kutokana na uwezo wao mkubwa katika kujibu maswali.

“Aweso we wajibu tu, waambie tutanini…lakini wabunge lazima mkubali kuwa waziri huyu anajibu maswali kwa ufasaha mkubwa na umaridadi, hongera kijana utafika mbali,” aliwahi kumsifia Zungu.

Lakini wakati hao wakijibu maswali hayo, Zungu hakuwa muumini wa majibu marefu yaliyotolewa na Wizara za Maliasili na Utalii pamoja na Kilimo na mara nyingi manaibu mawaziri walikutana na ‘mkwara mzito’ wa mbunge huyo wa Ilala akitaka wafupishe majibu yao.

Ni mwenyekiti wa tatu katika uwaziri

Zungu anakuwa mwenyekiti wa nne katika Bunge la 11 kuwa waziri.

Wengine ni George Simbachawene na Jenista Mhagama ambao waliwahi kuhudumu katika nafasi za wenyeviti wa Bunge lakini, Dk Mary Mwanjelwa ambaye amehudumu nafasi ya mwenyekiti katika bunge hili la 11 aliteuliwa kuwa naibu waziri.

Simbachawene (mambo ya ndani) na Mhagama (bunge, kazi, ajira na wenye ulemavu) walihudumu nafasi za mwenyekiti katika bunge la 10 chini ya Serikali ya Rais wa Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete.