Kitwanga afichua siri ya maono ya Rais Magufuli ujenzi wa miundombinu

Muktasari:

  • Ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza linalopita juu ya maji ya Ziwa Victoria lenye urefu wa Kilomita 3.2 ikiwa na barabara unganishi yenye urefu wa Kilomita 1.6 utagharimu zaidi ya Sh700 milioni.

Mwanza. Mbunge wa Misungwi (CCM, Charles Kitwanga amepongeza uthubutu wa Rais wa Tanzania, John Magufuli katika utekelezaji wa miradi mikubwa kwa fedha za mapato ya ndani.

Akisalimia wananchi wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi leo Jumamosi Desemba 7, 2019, Kitwanga amefichua siri ya uthubutu wa Rais Magufuli kuhusu ujenzi wa daraja la Mkapa wakati huo akiwa Naibu Waziri.

“Nakumbuka tuliomba fedha kutoka Kuwait lakini walipopelekewa maombi ya malipo ya awali ya dola 1 milioni wakaweka sharti la kulipwa kwanza deni la dola 10 milioni. Nakumbuka ulisema kama tunazo fedha hizo si ni bora kuzitumia kumlipa mkandarasi moja kwa moja,” amesema Kitwanga

Huku akikwepa kuingia kwa undani kwenye masuala na siri nyingi za uthubutu wa Rais Mafuguli, mbunge huyo maarufu kwa jina la ‘Mawe Matatu’ ametaja jinsi kiongozi huyo alivyofanikiwa kumshawishi Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa kuhusu kutumia fedha za ndani kujenga mtandao wa barabara kuunganisha mikoa yote ya Tanzania.

“Leo hii inaweka jiwe la msingi kujenga daraja lenye urefu mara tatu zaidi ya lile la Mkapa. Nisiseme mengi; itoshe tu kusema nina furaha sana na Mungu akulinde, akuongezee maisha marefu na afya njema. Sisi Misungwi tunasema tutakufia,” amesema Kitwanga aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania katika utawala huu wa Rais Magufuli

Huku akishangiliwa na wananchi, mbunge huyo ambaye eneo la mradi wa daraja la Kigongo-Busisi liko jimboni kwake ametumia fursa hiyo kumwalika Rais Magufuli kutembelea wilaya ya Misungwi akisema ni ombi alilopewa na wazee kuliwasilisha kwa mkuu huyo wa nchi.