Kizimbani kwa madai ya kujipatia mamilioni ili amuachie mtuhumiwa

Muktasari:

Perpetua Gondwe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matano ya kujipatia rushwa zaidi  ya Sh16 milioni ili amtoe, Edger Fuluga katika kituo cha polisi kati, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Perpetua Gondwe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matano ya kujipatia rushwa zaidi  ya Sh16 milioni ili amtoe, Edger Fuluga katika kituo cha polisi kati, jijini Dar es Salaam.

Akisoma hati ya mashtaka jana Ijumaa Februari 21, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu wakili wa Takukuru, Domonic Prudence amedai kati ya Januari 18, 2020 katika kituo hicho mshtakiwa alijipatia  Sh3.5 milioni kutoka kwa Scholastika Minja kwa niaba ya J1165PC, Wilbard Msaki ambaye ni mwajiliwa wa Jeshi la Polisi ili amuachie Edger Fuluga aliyekuwa anashikiliwa katika kituo hicho.

Katika  shtaka la pili inadaiwa Januari 19, 2020 mshtakiwa  alijipatia Sh2 milioni kutoka kwa Scholastika kwa niaba ya Msaki ili amwachie Fuluga.

Katika shtaka la tatu anadaiwa kujipatia Sh2 milioni kutoka kwa Scholastika kwa niaba ya Msaki ili amuachie Fuluga.

Shtaka la nne Januari 20, 2020 mshtakiwa huyo alijipatia Sh4.5 milioni kutoka kwa Scholastika kwa niaba ya Msaki ili amuachie Fuluga.

Ilielezwa kuwa katika shtaka la tano mshtakiwa alijipatia Sh2 milioni kutoka kwa Scholastika kwa niaba ya Msaki ili amwachie Fuluga.

Baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka umedai  upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mshtakiwa huyo ameachiwa kwa dhamana na kesi kuahirishwa hadi Machi 18, 2020 itakapotajwa tena.