Kocha Spurs aanza visingizio mapema

Muktasari:

Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino, amedai hana hakika kama kikosi chake kitakuwa na mafanikio kama cha msimu uliopita.


London, England. Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino amesema licha ya kutumia Pauni100 katika usajili wa majira ya kiangazi, lakini hana hakika na ubora wa kikosi chake.

“Nadhani unaweza kusema msimu uliopita tulikuwa na kikosi bora zaidi kwasababu tulicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema Pochettino.

Spurs iliweka rekodi yake kwa kumsajili kwa bei mbaya kiungo Tanguy Ndombele. Wengine ni Giovani Lo Celso (mkopo), Jack Clarke na Ryan Sessegnon na waliwabakiza Christian Eriksen, Danny Rose na Toby Alderweireld.

Wakati Pochettino akilalamikia ubora wa kikosi, Bournemouth imevunja mwiko dhidi ya wapinzani wao Southampton.

Ushindi wa mabao 3-1 iliyopata Bournemouth uliiweka katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England kabla ya mechi za jana Jumamosi.

Hii ni mara ya kwanza timu hiyo kuifunga Southampton. Mabao ya Nathan Ake, Harry Wilson na Callum Wilson yalitosha kuipa timu hiyo pointi tatu.

Bao la Southampton lilifungwa na Ward Prowse dakika ya 10 tu ya mchezo huo ambalo lilimpa matumaini Kocha Eddie Howe kabla ya kibao kugeuka.