Kompyuta yenye mfumo wa umeme Kenya, Zambia na Tanzania yapatikana

Kamanda Muroto akizungumza na wanahabari leo jijini Dodoma

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia  Boniface Mushi anayetuhumiwa kuiba kompyuta iliyokuwa imehifadhiwa mfumo wa umeme wa nchi za Tanzania, Kenya na Zambia.

Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia  Boniface Mushi anayetuhumiwa kuiba kompyuta iliyokuwa imehifadhiwa mfumo wa umeme wa nchi za Tanzania, Kenya na Zambia.

Polisi pia imekamata pikipiki nne zinazodaiwa kuwa za wizi, bunduki aina ya gobole mbili, mitambo ya kampuni ya Coca Cola na dawa za kuua wadudu.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 27, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema Mushi alikamatwa wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza baada ya mawasiliano yake kunaswa na kikosi cha polisi cha  makosa ya mtandao.

Mushi anadaiwa kuiba kompyuta hiyo mwanzoni mwa mwaka 2020  alipokuwa mlinzi wa kampuni binafsi ya QSS baada ya kuvunja ofisi za Tanesco mtaa wa Area D.

Muroto amesema Mushi angeweza kutumia kompyuta hiyo kuvuruga mfumo wa mtandao wa umeme wa nchi hizo.

“Nawapongeza vijana wetu wa mtandao pamoja na mkuu wa polisi Wilaya ya Kwimba, wamefanya kazi kubwa kusaidia chombo hiki muhimu kupatikana,” amesema Muroto.

Wakati huohuo, Muroto amesema wanawashikilia wahamiaji wanne na Watanzania waliokuwa wanawasafirisha wahamiaji hao.

Waliokamatwa ni Noor Shken, Ahmedasad Ahmed,Abdi Ahmed, Shueb Nadobe  na Abdrahiman Noor  ambao uraia wao haujafahamika. Watanzania waliokamatwa ni Yusuph Mohamed  na Idd Oka.