Komu, Selasini waibuka mkutano NCCR-Mageuzi, wasema hawatahamia CCM

Muktasari:

Wabunge wa Chadema, Joseph Selasini (Rombo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) leo Jumatano Februari 19, 2020 wameibuka katika mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi na kusema hawatahamia CCM.

Dar es Salaam.  Wabunge wa Chadema, Joseph Selasini (Rombo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) leo Jumatano Februari 19, 2020 wameibuka katika mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi na kusema hawatahamia CCM.

Wametoa kauli hiyo kutokana na kutajwa kuwa huenda nao wakahamia CCM baada ya ndani ya siku saba kushuhudiwa aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na Waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye wakihamia CCM baada ya kukaa Chadema kwa takribani miaka mitano.

Komu ambaye alialikwa katika mkutano pamoja na Selasini, amesema bado ni mwanachama wa Chadema na endapo ataamua kuondoka katika chama hicho hatakuwa tayari kuhamia  CCM.

“Sina rekodi ya kuwa CCM kama ninavyofananishwa na wengine, mwaka 1988 ili uwe kiongozi wa chuo cha  UDSM (Chuo Kikuu Dar es Salaam) ilikuwa lazima upitishwe Lumumba lakini tulikataa, tukaingia kwenye uchaguzi na kushinda tukarejesha Duso, sasa inaitwa Daruso (Serikali ya Wanafunzi UDSM).”

“Sasa kama chama kikinishinda siendi Lumumba, kushindwa Chadema ni kawaida kwa sababu vyama siyo mama yetu kwa mfano Mbatia akitaka kwenda aende tuone NCCR kama chama hakitaendelea,” amesema Komu.

Lumumba ni mtaa uliopo jijini Dar es Salaam zilipo ofisi ndogo za CCM.

Katika maelezo yake Komu amesema, “Profesa Ibrahim Lipumba aliondoka CUF mwaka  2015 lakini CUF ikaimarika. Dk Willbrod Slaa aliondoka Chadema mwaka 2015 ikaimarika zaidi, kwa hiyo vyama ni mali ya wanachama, wanachama ni roho ya vyama. Niwaambie watu wa Moshi kama Chadema kutanishinda, nguvu zangu nitazipeleka kwingine kuimarisha upinzani zaidi.”

Kwa upande wake Selasini amesema, “msiogope (wanachama NCCR) mko sehemu sahihi. Mimi nina hasira za kuchafuliwa na tuhuma za kwenda CCM.”