Kubenea amtaka Dk Mpango kuacha ushabiki wa kisiasa

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Ubungo (Chadema) Saed Kubenea amekosoa kauli aliyoitoa Waziri wa Fedha na Mpango Dk Philip Mpango aliyosema mgombea bora atatoka CCM na kumtaka kujielekeza kwenye ukusanyaji wa mapato ili kulisaidia taifa.


Dodoma. Mbunge wa Ubungo (Chadema) Saed Kubenea amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kukukusanya fedha kwa ajili ya kuliendeleza Taifa na kuacha ushabiki wa kisiasa.

Kubenea ameyasema hayo leo Jumanne Juni 18, 2019 wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya Tanzania mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Amesema wakati Dk Mpango anawasilisha bajeti Alhamisi  iliyopita ya Juni 13, 2019 aliacha jukumu la kusimamia sera za Serikali ya Tanzania juu ya bajeti na akahamia kwenye ushabiki wa kushabikia chama chake cha CCM.

Kubenea amesema Taifa ni changa sana na kwamba hawana mahali popote pa kwenda kwa sababu wamezaliwa, wamekulia Tanzania.

“Hatujawahi kwenda hata nchi za watu kuishi kwa miaka 10 kwa hiyo hatuna mahali pa kwenda. Bila kutuliza, kuheshimu amani yetu busara zetu hakika tunaweza kulipeleka Taifa hili mahali pabaya sana,” amesema.

Amesema jukumu la Dk Mpango ni kusimamia mapato ya Serikali na kulitoa Taifa hapa lilipo nakuachana kabisa na ushabiki wa kisiasa.

Amesema katika mwaka wa fedha 2019/20 imetenga ni Sh12.25 trilioni sawa na asilimia 37 ya bajeti, fedha karibu zote zimekwenda katika miradi isiyozidi minne.

“Lakini mheshimiwa uchumi wetu uweze kukuwa ungewekeza katika kilimo, viwanda umwagiliaji lakini bajeti za wizara zote ziko chini ya asilimia 5,”amesema.