Kumekucha... Sven ashtuka aleta tatu kali

Muktasari:

Simba itakuwa wageni wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara na kikosi cha timu kilitarajiwa kuondoka saa 12:30 leo asubuhi kuwahi pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

KASI ya straika Chris Mugalu katika kutupia mabao kambani imelikuna benchi la ufundi la Simba na sasa ameachiwa msala kwenye mechi yao dhidi ya Tanzania Prisons itakayopigwa Alhamisi, huku Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck akitamba kutumia mifumo mitatu tofauti ili kushinda ugenini.

Simba itakuwa wageni wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara na kikosi cha timu kilitarajiwa kuondoka saa 12:30 leo asubuhi kuwahi pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

Kocha Sven, aliliambia Mwanaspoti juzi mara baada ya mechi yao kirafiki dhidi ya Mlandege ambapo Mugalu alitupia mabao mawili wakati Simba ikishinda 3-1 kuwa, katika kuhakikisha wanapata ushindi ugenini dhidi ya Prisons, imefanyia kazi mifumo mitatu tofauti ya kimbinu.

Sven aliyekiri kukunwa na uwezo wa Mugalu katika kufunga mabao alisema; “Kila mechi tunayocheza ugenini ni ngumu na wapinzani wanakuwa wamehamasika kwa asilimia mia moja. Iwe ni Ihefu, Mbeya City na hata hao Prisons.”

“Tunajua tunakwenda kukutana na ugumu kwani kila mechi ni ngumu. Tutasafiri na wachezaji 22 na wachache hawatosafiri kwa sababu tofauti. Wengine kwa masuala ya kifamilia na baadhi kwa sababu ndogondogo,” alisema Sven na kuongeza;.

“Tunaenda kucheza mechi moja tu, hivyo hakuna haja ya kusafiri na wachezaji wengi na hiyo inasaidia kuondoa hisia hasi kwani wengine wanaweza kulalamika kwamba kwa nini tumesafiri lakini hatujacheza.”

Wachezaji ambao huenda wasisafiri ni Pascal Wawa na Clatous Chama waliorudi makwao kufuatilia hati za kusafiria, John Bocco, Erasto Nyoni ambao wameanza mazoezi mepesi pamoja na Meddie Kagere na Ibrahim Ame ambao ni majeruhi kama ilivyo kwa Gerson Fraga.

Kukosekana kwa Kagere na Bocco ina maana msala mzima wa mechi hiyo umeachwa kwa Mugalu ili kuhakikisha Simba inaibuka na ushindi na Kocha Sven amepanga kutumia mifumo mitatu au yote ambayo ameifanyia kazi katika maandalizi yao ikiwemo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege.

Kwa kuanzia, Simba inaweza kuutumia mfumo wake inaopendelea kuutumia wa 4-2-3-1 ambao mara ya mwisho iliutumia dhidi ya Gwambina FC iliposhinda kwa mabao 3-0.

Lakini baada ya hapo Simba ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-0, ilibadilika na kutumia mfumo wa 4-4-2 ambao ilisimamisha washambuliaji wawili wa kati, Meddie Kagere na Chris Mugalu huku pia ikitumia mawinga wawili.

Lakini katika mchezo wa juzi dhidi ya Mlandege, Simba ilibadilika kidogo na licha ya kucheza mfumo wa 4-4-2, safari hii ilimtumia kiungo mmoja tu mkabaji ambaye mbele yake ilipangwa viungo watatu wa ushambuliaji na pia kukawepo na washambuliaji wawili wa kati ambao ni Mugalu aliyepangwa pamoja na Bernard Morrison.

Kocha Sven, alisema aliamua kubadili mfumo dhidi ya Mlandege kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji ingawa anaweza kuutumia huohuo au mingine miwili aliyotumia katika mechi zilizopita.

“Leo (juzi) dhidi ya Mlandege nilitumia kiungo mmoja mkabaji, lakini asubuhi tulicheza mechi ya kirafiki na kikosi cha vijana na nilipanga viungo wawili katika eneo hilo kama ilivyo kawaida,” alisema. “Nimelazimika kufanya hivi kwa sababu kuna wachezaji tumewakosa, japo ninao wengine kama wanne hivi wanaoweza kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji. Hata hivyo mfumo wowote unaweza kutumika, ili kupata ushindi kwenye mechi hiyo ya ugenini,” alisisitiza Sven.

MUGALU HUYU HAPA

Naye Mugalu kwa upande wake alisema Simba inataka kushinda mechi hiyo ya Prisons ili kudhihirisha ukubwa wao na kwa bahati anafurahi kuwepo kwenye kikosi bora chenye kiu ya mafanikio.

“Mechi itakuwa ngumu, lakini Simba ni timu kubwa na inatakiwa kupata ushindi popote pale na dhidi ya timu yoyote, hivyo tunakwenda kupambana na Prisons tukiwa na lengo la kuibuka na ushindi,” alisema Mugalu ambaye alisema kama mshambuliaji wajaibu wake ni kufunga kila anapopata nafasi.

“Kufunga ni kazi ya mshambuliaji, bado tuna kazi kubwa kuhakikisha tunatetea ubingwa, hivyo lazima tutumie nafasi tunazotengeneza, ndio maana nafunga ingawa bado sijaridhika,” alisema mshambuliaji huyo. Mugalu amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu mpaka sasa, huku akiwa na rekodi nzuri ya kucheza na kufunga kwa kila mechi aliyoichezea Simba kwenye ligi na manne katika michezo ya kirafiki akiwa ndiye kinara kwa sasa kwa wachezaji wote ndani ya msimu huu akiwa na mabao saba.