Kuvuka Kigongo–Busisi Mwanza dakika nne

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi litakalokuwa la sita kwa ukubwa Afrika lenye upana wa mita 28.4  na urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.65 litakalogharimu Sh700 bilioni


Mwanza. Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi jijini Mwanza nchini Tanzania siyo tu kutaondoa adha ya kusubiri na kutumia vivuko, bali pia kutapunguza muda wa kuvuka eneo hilo kutoka wastani wa dakika 40 hadi saa mbili hadi kufikia dakika nne.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Desemba 7, 2019 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi.

Daraja hilo litaunganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema za mkoa wa Mwanza nchini Tanzania pamoja na mikoa ya Mwanza na Geita ujenzi wake utagharimu Sh700 bilioni.

Utakapokamilika, daraja hilo ambalo pia linaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) litakuwa na urefu wa Kilomita 3.2 likipita juu ya Ziwa Victoria.

Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara unganishi wenye urefu wa Kilomita 1.6 na fedha zote za utekelezaji zinatokana na mapato ya ndani.

Mfugale amesema daraja hilo ni la sita Afrika likitanguliwa na la Misri likiwa na urefu wa kilomita 20.5, ikifuatiwa na lililoko nchini Nigeria lenye urefu wa kilomita 11.

Madaraja mengine marefu na kilomita zake kwenye mabano ni Suecanal lenye kilomita 3.9 na mengine mawili yiliyoko nchini Msumbiji yenye urefu wa kilomita 3.8 na 3.6. 

Alipotangaza uamuzi wa kujenga daraja eneo hilo wakati wa ziara zake kadhaa mkoani Mwanza, Rais Magufuli alisema kukamilika kwa mradi huo siyo tu kutarahisisha usafiri na usafirishaji, bali pia kutoandoa adha ya wagonjwa kupoteza maisha wakati wakisubiri vivuko vinavyotoa huduma eneo hilo.

Eneo la Kigongo – Busisi linahudumiwa na vivuko viwili vya Mv Mwanza ambacho ni kipya na Mv Misungwi ambazo hutumia wastani wa dakika 30 hadi 40 kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine.

“Kila siku watu wamekuwa wakisubiri feri (kwa muda mrefu) ...haiwezekani kila siku tunategemea feri. Anafika pale mama mjamzito mpaka ukasubiri feri; uchungu utakusubiri wakati mtoto anataka atoke? Pale wameshakufa watu.” amewahi kukaririwa akisema Rais Magufuli

“Tumeomba fedha kutoka kwa wafadhili tumekosa. Tumeamua tunajenga kwa fedha zetu wenyewe,”