LIVE: Magufuli atua JNIA kuzindua Rada zitakazookoa fedha, usalama Dar

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Rais wa Tanzania,  John Magufuli wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya kushiriki uzinduzi wa rada mbili za kuongozea ndege.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Rais wa Tanzania,  John Magufuli wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya kushiriki uzinduzi wa rada mbili za kuongozea ndege.

Uzinduzi huo unafanyika leo Jumatatu Septemba 16, 2019 na kuongozwa na Magufuli.

Mbali na Rais Magufuli viongozi  wa dini, mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi na watendaji wa Serikali ni miongoni mwa walioshiriki uzinduzi huo.

Kuzinduliwa kwa rada hizo kutasaidia Tanzania kuacha kutumia mamilioni ya fedha kuzilipa nchi jirani sanjari kulinda anga lote la nchi tofauti na awali. Uamuzi huyo ulitolewa baada ya Tanzania  kukosa rada zenye uwezo unaokubalika kimataifa.

Kufungwa kwa rada hizo kutawezesha kukusanya Sh1bilioni ilizokuwa ikipotelea  kwa Kenya inayolinda asilimia 75 ya anga la Tanzania.

Tanzania ilikuwa inapoteza fedha hizo kwa miaka 41 sasa baada ya Shirika la Anga Duniani (ICAO) kuipa Kenya jukumu la kulinda anga la Ukanda wa Afrika Mashariki linalojumuisha nchi za Tanzania, Madagasca, Mauritius, Comoro na Visiwa vya Mayotte.