VIDEO: Wakuu wa nchi Sadc wasaini itifaki nne

Muktasari:

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ambaye ni Rais wa Tanzania, John Magufuli  amewaongoza wakuu wa nchi 16 za jumuiya hiyo kusaini marekebisho katika itifaki nne

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ambaye ni Rais wa Tanzania, John Magufuli  amewaongoza wakuu wa nchi 16 za jumuiya hiyo kusaini marekebisho katika itifaki nne.

Itifaki zilizosainiwa ni  kuhusu maendeleo ya viwanda, kubadilishana watuhumiwa na wafungwa na masuala ya jinai.

Sekretarieti ya Sadc itafuatilia utekelezaji wake kwa nchi zote zilizotia saini.

Makubaliano hayo yamefanyika leo Jumapili Agosti 18, 2019 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).

Tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 1992, itifaki 33 zimeshasainiwa na wakuu wa nchi hizo.

Hata hivyo si lazima kwa nchi kusaini itifaki zinazopitishwa na mtangamano huo hadi pale nchi husika itakapojiridhisha au kuwa tayari kusaini hapo baadaye.