Laini za simu kuzimwa kwa awamu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba amesema uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole unafanyika kwa awamu kuanzia jana Jumatatu Januari 20, 2020 ili kuondoa usumbufu.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba amesema uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole unafanyika kwa awamu kuanzia jana Jumatatu Januari 20, 2020 ili kuondoa usumbufu.

Amesema hadi jana saa  nne usiku walikuwa wamezima laini 975,041.

Amesema kundi la kwanza waliozimiwa laini ni watu 656,091 ambao wana vitambulisho vya Taifa au namba lakini hawajasajili laini zao.

Kilaba amesema kundi la pili ni watu 318,950 waliosajili laini zao kwa kitambulisho cha Taifa kabla ya kuanza mfumo wa kusajili kwa alama za kidole.

“Hawa wote hawana sababu ya kutozimiwa laini zao leo, uzimaji huu hatutaki kumnyang’anya mtu laini yake ambayo ameizoea ila tutaisitisha kutoa na kupokea huduma. Hivyo simu yake itapokea ujumbe mfupi tu ambao utakuwa unamkumbusha usajili” amesema Kilaba akibainisha kuwa  usajili wa laini za simu hauna kikomo.

Ameongeza, “tunazima kidogo kwa sababu ya mambo ya kitaalamu, hauwezi ukazima laini milioni tano au  10 kwa mara moja.”

“Tunahitaji warudi, tukiwazimia tunategemea kesho watarudi kwenye foleni za kuhuisha laini zao kwa hiyo wakienda wengi zaidi hawatapata huduma kama ambavyo walijaa juzi na jana na leo mpaka mifumo ya Nida inaelemewa.”

Amesisitiza kuwa watafanya kistaarabu na kiufundi uzimaji laini ili mifumo isielemewe kwenye usajili.